MKUU wa Mkoa wa Tanga Mhe Balozi Dk Batilda Burian, ameitaka polisi mkoani hapa, kuepuka vitendo vinavyoweza
kuwaingiza katika kashfa za rushwa, badala yake wafanye kazi kwa misingi ya haki na weledi.
Amesema hayo kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti na tuzo, askari polisi saba waliofanya kazi vizuri hususani katika kuchunguza na kuzuia uhalifu kweny maeneo yao ya kazi.
“Fanyeni kazi kwa haki na weledi mkizingatia tunu za taifa letu, ili matukio tunayoyaona kwa wenzetu yasitokee nchini kwetu,”amesema.
Mhe Balozi Dk Batilda amesema polisi wakitekeleza majukumu yao kwa haki, weledi na kutumia mbinu bunifu za kisayansi kupambana na uhalifu, kutaongeza sifa kwa jeshi
hilo.
Pia ameiagiza polisi mkoani hapa kuendelea kudhibiti uhalifu ukiwemo wa mtandaoni kama ilivyotokea kwa vijana wa Q-net waliokamatwa hivi karibuni.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, ACP Maket Msangi, amethibitisha kuyapokea na kuyafanyia kazi maagizo ya Mhe Balozi Dk Batilda, na kuahidi kuendelea kupambana na uhalifu wa aina zote.