Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-20234) ili kufikia malengo ya utunzaji wa mazingira.
Ametoa kauli hiyo wakati akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 15 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 28 Juni, 2024 akisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi mbali ya kuimarisha utunzaji wa mazingira pia yataboresha afya na ustawi wa jamii.
“Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa wizara za kisekta, Taasisi, Idara za Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Asasi za kiraia, Sekta binafsi, Wadau wa maendeleo, Wabunge na Watanzania wote kushiriki katika utekelezaji wa mkakati huu,“ amesema.
Waziri Mkuu amesema kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inaendelea kote nchini na tayari maelekezo thabiti yameshatolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Ameongeza kuwa Miongozo iliyotolewa inaendelea kusimamiwa kikamilifu sanjari na utoaji wa elimu ili wananchi wapate uelewa na hivyo kuachana na matumizi ya nishati chafu ambayo yanachangia ukataji wa miti kwa lengo la kupata kuni na mkaa.
Inakadiriwa kuwa takribani hekta 469,000 za misitu hupotea kila mwaka wakati nishati za kuni na mkaa zikitajwa kuwa ni chanzo kikuu cha kutoweka kwa misitu hiyo.
Itakumbukwa kuwa Mkakati huu ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 08 Mei, 2024 ukitoa mwongozo wa kitaifa kwa wadau wote kuhakikisha nchi inafikia lengo ililojiwekea la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Halikadhalika, lengo la Mkakati huo likitekelezwa na kutimia litapunguza gharama ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuongeza upatikanaji na uwekezaji wa nishati hiyo.
Bunge limeahirishwa hadi tarehe 27 Agosti, 2024 ambapo katika mkutano wa 15 lilipitisha Bajeti Kuu ya Serikali ya kiasi cha shilingi trilioni 49.35 kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambayo pamoja na mambo mbalimbali pia inaakisi sekta ya mazingira.