Na Mwandishi wetu, Babati
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Babati,mkoa wa Manyara, Anna Mbogo ameipongeza Taasisi ya Tembo pilipili kwa kuwezesha vikundi 25 vya wakulima toka eneo la Ziwa Manyara, Tarangire na Ngorongoro kunufaika na mikopo yenye jumla ya shilingi 125 milioni kwa kipindi cha mwaka 2023.
Amesema hayo katika kongamano la kuzuia tembo kwa njia ya pilipili ili wasiweze kuvamia mashamba na kuharibu mazao, kongamano lililoandaliwa na Tembo pilipili program Katika Kijiji cha Mayoka kata ya Magara wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Amesema vikundi vya wakulima vina mchango mkubwa katika kuongezeka kwa wanyamapori na uhifadhi wa mazingira kwa sababu vinatumia njia rafiki ya kuzuia Tembo kuvamia mashamba kwa kupaka pilipili katika uzio wa mashamba na hivyo kumfanya tembo asiweze kuingia katika mashamba hayo na kuharibu mazao.
“Tukiweka uzio wa pilipili katika mashamba yetu tutazuia tembo kuvamia kwani wajua sio maeneo rafiki kwao na hivyo hawataweza kuingia katika mashamba, lakini pia tunashauriwa na wataalamu kulima mazao mbadala ambayo tembo hali majani yake” alisema Mbogo.
Alisema wakulima hao wanapaswa kupanga nyanda za malisho ya mifugo ili kuepuka kulisha mifugo katika maeneo ya hifadhi ya wanyamapori kwani husababisha kuambukizana magonjwa kati ya Wanyama wafugwao na wanyamapori.
Awali Afisa Utalii na uhifadhi wilaya ya Babati Christopher Laizer amesema serikali ina mkakati wa kujenga kituo Cha Ulinzi wa wanyamapori (Ranger Post) katika maeneo yenye Tembo waharibifu wa mazao ili kuhakikisha wakulima hawapati hasara ya mazao yao na kwa wilaya ya babati kitajengwa katika kata ya Endakiso.
Amesema kwa sasa wananchi wamepata uelewa mkubwa kutumia uzio wa pilipili katika mashamba yao na kuwazuia tembo wasivamie mashamba na hivyo kuwa na uhakika wa kuvuna mazao yao bila kuathiriwa na tembo waharibifu.
Mkurugenzi wa Tembo pilipili program Dk. Alex Chang’a amesema walianzisha shirika hilo kushirikiana na wakulima katika kukabiliana na wanyamapori waharibifu wa mazao husuani tembo na tangu kuanzishwa kwa mradi wa tembo pilipili jumla ya wakulima 3600 toka vikundi 120 vya Tarangire, Lake Manyara na Ngorongoro vimenufaika kwa kuweka uzio wa pilipili na sasa mazao yao hayavamiwi na tembo hivyo kuwana uhakika wa kuvuna mazao.
Amewashauri wakulima nchini kutumia uzio wa pilipili, tofali la pilipili na walime mazao ya pilipili kwa sababu pilipili hailiwi na tembo na ni malighafi muhimu na rafiki ya kuzuia tembo.
Amesema kuwa watu wanaoishi kjaribu na hifadhi wanapoteza mali zao za kiuchumi, wanapoteza Maisha, wanajeruhiwa na tembo wakiingia shambani au kwenye maeneo ya makzi yao ndiyo maana walikuja na mradi wa kudhibiti tembo kwa njia ya pilipili ambayo ni rafiki kwa mazingira, ambayo mwitikio wake ni mzuri isipokuwa changamotio ya ukosefu wa mitaji ili wakulima waweke uzio na wawekeze kwenye kilimo na ufugaji ili kujiongezea kipato cha familia.
Amesema Pamoja na kuwapa elimu ya matumizi ya pilipili katika kudhibiti tembo waharibifu hiviwezesha vikundi hivyo elimu ya ujasiriamali na kisha kuwatafutia mikopo toka taasisi ya vision fund kuwakopehsa wakulima hao ili waweze kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo na baoshara nyingine zinazowaongezea kipato cha familia.
Katika kongamano hilo wakulima hao walifundishwa pia jinsi ya kutumia mabomu ya kufukuza tembo waharibifu wa mazao mashambani toka kwa mtaalamu wa tawiri…… ambapo walipewa njia za kupata vibali vya kuwa bna mabomu hayo na jinsi ya kuyatumia kufukuza tembo.