●Zapongeza ukuaji wa Sekta ya Madini Tanzania
●Zafurahishwa na Ushirikishwaji wa vyama vya uchimbaji madini.
*Dodoma*
Ukuaji na Maendeleo ya Sekta ya Madini Tanzania umezivutia nchi nne za Kenya , Uganda , Zambia na Msumbiji kuja kujifunza Usimamizi wa Rasilimali madini na kubadilishana uzoefu kuhusu uchimbaji endelevu.
Hayo yalibainishwa na Naibu Katibu Mkuu wizara ya madini, Msafiri Mbibo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la _Africa Resilience Dialogue_ (ARD) lililofanyika Jijini Dodoma Juni 27, 2024 .
Akielezea kuhusu ukuaji wa Sekta ya Madini Tanzania Mbibo alisema kuwa, kufikia 2023 sekta ilikuwa kwa asilimia 11.3 kutoka asilimia 10.8 kwa mwaka 2022.
Mbibo alifafanua kuwa, sekta ya madini ni miongoni mwa sekta za uziduaji ambazo kama hazitafanyika kwa uangalifu zinaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na hivyo kuathiri afya na usalama wa wananchi wa maeneo husika.
Kuhusu usimamizi wa sekta Mbibo alieleza kuwa, Wizara ya madini imeendelea kusimamia ushiriki wa wadau mbalimbali vikiwemo Vyama vya Wachimbaji wadogo kama vile TwiMMI na TAWOMA ili kuhakikisha kwamba wanawake wananufaika ipasavyo katika mnyororo mzima wa sekta ya madini.
Sambamba na ushiriki wa kisekta kimataifa , Mbibo aliongeza kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa Jumuhiya ya _Extractive Industry Transparency Initiative (_ EITI) ambapo mikataba na mapato yote ya sekta za Uziduaji ikiwemo sekta ya madini huwekwa wazi kwa wananchi na nchi ambazo ni jumuhiyo wanachama.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini (TWiMMI) , Paulina Ninje alipongeza jinsi sekta ya madini inavyotoa ushirikiano mkubwa kwa vyama vya wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji madini nchini.
Ninje aliongeza kuwa kwasasa chama cha TwiMMI kina miradi mbalimbali na kimefanikiwa kuwapatia vifaa vya uchimbaji madini kwa wanawake 150 wanaojishughulisha na uchimbaji madini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chama kinachojishulisha na Utoaji wa elimu ya mazingira na Uwajibikaji wa Jamii (PDI), Alpha Ntayomba alisema kuwa wanafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na taasisi ya TwiMMI katika kutoa elimu ya kuhifadhi mazingira , Uwajibikaji wa jamii na Haki za Binadamu.
Kongamano hilo la siku moja lilijumuhisha wadau kutoka sekta binafsi na sekta za Umma kutoka nchi washiriki.