Dar es Salaam,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema kuanzishwa kwa Masoko ya Madini hapa nchini kumesaidia kuondokana na utoroshaji wa madini hali iliyopelekea kuongezeka kwa mchango wa Wachimbaji Wadogo katika uzalishaji wa dhahabu nchini kutoka chini ya asilimia 5 na kufikia asilimia 40.
Amesema hayo leo Juni 28, 2024 wakati akizungumza katika mdahalo maalum wa Hoja yako Mezani ulioandaliwa na Taasisi ya Hakirasilimali na kufanyika katika Hoteli ya Seashells Millenium Jijini Dar es Salaam. Mdahalo huo ulijikita katika mada kuu ya kubainisha maeneo yanayoonesha viashiria vya uchimbaji haramu wa madini.
Mbibo ameeleza kuwa Wizara kupitia Tume ya Madini imechukua hatua madhubuti kudhibiti utoroshaji wa madini. Hatua hizo ni pamoja na kuanzisha masoko ya madini mwaka 2019, ambayo yamewapa wachimbaji wadogo soko la uhakika na bei nzuri zinazoshabihiana na bei ya soko la dunia, na kupelekea mchango wa wachimbaji wadogo katika uzalishaji wa dhahabu nchini kuongezeka kutoka chini ya asilimia 5 na kufikia takriban asilimia 40.
Aidha, amesema kuwa ukaguzi kwenye mipaka ya nchi na viwanja vya ndege umeimarishwa kwa kuweka watumishi wenye weledi na vifaa vya kisasa ili kudhibiti utoroshaji, sambamba na viwango vya tozo na kodi mbalimbali kwa wachimbaji wadogo kupitiwa upya mara kwa mara ili kuwafanya wasishawishike kutorosha madini nje ya nchi, lakini pia uwepo wa kikosi kazi maalumu umesaidia kusimamia na kudhibiti utoroshaji wa madini.
Katika hatua nyingine, Mbibo amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria ya Madini Sura ya 123, mtu au taasisi yeyote hairuhusiwi kufanya utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji au biashara ya madini bila leseni halali na kubainisha kuwa hata hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakijihusisha na uchimbaji bila leseni halali.
Na kuongeza kwamba, Wizara kupitia Tume ya Madini imefanya jitihada kubwa kuhakikisha wachimbaji wote wanatimiza matakwa ya sheria hii, ikiwa ni pamoja na urasimishaji wa wachimbaji wasio rasmi na kutenga maeneo maalumu kwa wachimbaji wadogo.
Vilevile, Mbibo ameeleza kuwa sheria za kimataifa zinazuia biashara ya madini kutoka nchi zenye vita na machafuko, na kwamba Tanzania imefanikiwa kuondoa uwepo wa madini haramu kutoka nchi hizo kupitia mfumo wa biashara ya madini kwenye masoko yaliyoanzishwa, ambapo hatua zote za biashara zinajulikana na hufuatwa kwa uhalali.
Akizungumzia Matumizi ya Zebaki (Mercury) Mbibo amesema, Tanzania ni moja ya nchi zilizokubaliana na makubaliano ya Minamata ya kudhibiti matumizi ya zebaki ambayo yana madhara mengi kwenye mazingira. Wizara imehakikisha matumizi ya teknolojia mbadala na rafiki kwa mazingira katika uchenjuaji wa madini, kama vile teknolojia mpya ya kutumia cyanide.
Kuhusu ajira za watoto kwenye Migodi, Mbibo amesema, Sheria mbalimbali za kimataifa na za hapa nchini zinakataza ajira za watoto chini ya umri wa miaka 18, na kwamba, Wizara na taasisi zake zinasimamia utekelezaji wa sheria hizo kuhakikisha haki za binadamu na utawala bora unazingatiwa katika sekta ya madini.
Pia, kupitia mdahalo huo, Mbibo ameeleza juhudi za serikali katika kuhakikisha uchimbaji wa madini hapa nchini unazingatia afya, usalama, na uendelevu wa mazingira unapiga vita uchimbaji haramu na usio rafiki kwa mazingira.