Na Mwamvua Mwinyi, Pwani, Juni 28
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Mkoani Pwani kimeelekeza vikao vya uteuzi vikatende haki,kuteua wagombea wanaokubalika na wenye sifa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024.
Aidha Halmashauri Kuu hiyo ,imetoa maelekezo kuhakikisha ujenzi wa jengo la kitega uchumi na ofisi za CCM Mkoani humo unakamilika na kuanza kutumika ifikapo Julai 30.
Akielezea maazimio ya agenda zilizojadiliwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoani Pwani ,Katibu wa CCM mkoani humo Bernard Ghaty alieleza ,wameweka mpango kuhakikisha wanapata wagombea wanaokubalika kwa umma.
Alielezea kuwa, wameelekeza vikao vya chama vya uteuzi vikatende haki na kusisitiza kuchagua wagombea wenye sifa na uwezo.
Ghaty aliwataka wanaCCM kuendelea kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa ilani katika sekta ya elimu,maji, miundombinu ya barabara,umeme nk.
Kuhusu jengo la kuimarisha uchumi wa chama mkoa, Ghaty alieleza, ujenzi umefikia asilimia 80, ambapo hadi kukamilika kwake litagharimu milioni 500.
Katibu huyo alieleza kuwa ,hadi sasa wametumia milioni 246 na ujenzi unaendelea kwa hatua mbalimbali.
“Ujenzi huo una pande mbili,upande wa kitega uchumi na ofisi za CCM,” Tunajivunia uwepo wa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan, wakati tunapambana na ujenzi huu wa jengo hili la kisasa, yeye pia kuna sehemu ya nguvu yake “alielezea Ghaty.
Awali akitoa taarifa ya kiserikali, Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alipongeza Serikali kuu kwa utekelezaji wa ilani na kuelekeza fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo mkoani hapo.
Kunenge alieleza, ujenzi wa jengo la kisasa la CCM mkoa limefikia asilimia 80.
Kuhusu miundombinu ya barabara alibainisha kwamba, licha ya mvua kubwa zilizonyesha ,lakini Serikali mkoa na Serikali Kuu zinahakikisha maeneo yote yanapitika na ukarabati unaendelea.
Katika kikao hicho ,pamoja na mambo mengine kilijadili hali ya kisiasa mkoani humo na kupata taarifa ya kiserikali namna miradi inayotekelezwa.