Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akifungua kongamano la tano la kitaifa la wafanyakazi na washiriki wa afya ya macho Tanzania katika Hoteli ya Verde, Mtoni Mkoa wa Mjini-Magharibi.
Waziri wa Afya Zanzibar, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui akizungumza kuhusiana na huduma za macho katika kongamano la tano la kitaifa la wafanyakazi na washiriki wa afya ya macho Tanzania katika Hoteli ya Verde, Mtoni Mkoa wa Mjini-Magharibi .
Rais wa chama cha madaktari bingwa wa mcho Tanzania Dr Christopher Mwanansao akitoa salamu za chama hicho katika mkutano wa tano wa kitaifa wawafanyakazi na washiriki wa afya ya macho Tanzania katika Hoteli ya Verde, Mtoni Mkoa wa Mjini-Magharibi. PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO
…….
Na Fauzia Mussa, Maelezo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema endapo wataalamu wa matibabu ya macho watatumia taaluma zao ipasavyo itasaidia kutatua changamoto zinazoikabili Jamii, zikiwemo za Ustawi na huduma bora za Afya.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akifungua kongamano la tano la kitaifa la chama cha madaktari bingwa wa macho Tanzania (TOS) katika Hoteli ya Verde, Mtoni Mkoa wa Mjini-Magharibi, kwa niaba ya Dkt Mwinyi amesema kufanya hivyo pia kutapelekea Nchi zinazoendelea kuyafikia Maendeleo Endelevu.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya, itaendelea kushirikiana na chama hicho ili kuondokana na baadhi ya changamoto zinazowakabili jambo ambalo wawezesha wananchi kuendelea kupata huduma kikamilifu kutoka kwa wataalamu hao.
Aidha Dkt Mwinyi aliutaka uongozi wa chama hicho kutafuta uhusiano na Mashirika mengine ya Kimataifa ili kuwasaidia wanachama wao kuongeza ujuzi , uzoefu wa taaluma yao na kuleta mabadiliko chanya ya Huduma za Macho nchini.
Mapema aliwapongeza Wanachama wa TOS kwa kuandaa kambi ya macho kama sehemu ya shughuli ya maadhimisho ya mkutano huo jambo mbalo limesaidia kupatiwa matibabu ya haraka kwa Wananchi waliojitokeza.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui, amewashauri Vijana kusomea taaluma ya Utabibu wa Maradhi ya Macho, kwani Mahitaji ni makubwa kutokana na ongezeko za Hospitali Mpya za Kisasa, pamoja na wagonjwa wa macho kuwa wengi Nchini.
Aidha amesema Wizara inaendelea kuongeza wataalamu wa fani hiyo na kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa lengo la kutoa huduma bora kwa jamii.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Habiba Omar amesema katika kuimarisha huduma za macho nchini Wizara itaendelea kuwafikia Wananchi wote wenye matatzo hayo ili kupunguza athari za uoni.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha januari hadi disemba 2023 zaidi ya watu elf kumi na tano walipatiwa huduma za macho katika kliniki mbalimbali unguja na Pemba.
Akitoa salamu za chama cha madaktari bingwa wa macho Tanzania Rais wa Chama hicho Dr. Christopher Mwanansao amesema kongamano hilo liliambatana na utoaji wa huduma kwa jamii ambapo chama kiliendesha kambi maalum ya siku nne na kufanikiwa kuchunguza Zaidi ya watu elfu moja, kufanya upasuaji kwa wagonjwa Zaidi ya 160 ukiwemo upasuaji wa kawaida na wa kisasa wa kutoa mtoto wa jicho kwa kutumia matundu madogo.
amesema katika kambi hiyo idadi kubwa ya wananchi waligundulika kusumbuliwa na presha ya macho na kusema ipo haja ya chama hicho kushirikiana na serikali kufanya tafiti Zaidi juu ya tatizo hilo.
Alifahamisha kuwa lengo la chama hicho ni kushirikiana na serikali katika kuimarisha huduma za macho, kufanya tafiti na kuwaunganisha wadau mbalimbali wa afya ya macho , ambapo aliahidi kuendeleza mashirikiano hayo ili malengo yaweze kufikiwa.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Watoa-huduma za Matibabu ya Macho, Wataalamu wa Afya na Madaktari Bingwa kutoka Mataifa mbali mbali yakiwemo ya Korea, India, Marekani na Wenyeji Tanzania Bara na Zanzibar.
Kabla ya hafla hiyo, Mheshimiwa Othman alitembelea Maonyesho ya wafanyabiashara mbali mbali wa sekta ya macho kutoka Taasisi za Ndani na Nje ya Nchi yaliyolenga kutoa fursa ya kuwaunganisha watu hao kuweza kuleta bidhaa zinazokidhi mahitaji ya huduma hiyo.