Mbunge wa Bunge la EALA nchini Tanzania,J ames Ole Millya akizungumza Bungeni
Mbunge wa Bunge la EALA kutoka Tanzania DkT. Abdullah Makame akielezea kuhusiana na bajeti hiyo.
Spika wa Bunge la EALA, Joseph Ntakirutimana akizungumza bungeni hapo na wabunge wa EALA.
…………
Happy Lazaro,Arusha .
Wabunge wa bunge la Afrika Mshariki (EALA) wameshauri Viongozi wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika kusaidia kuzungumza na nchi ambazo bado zinasuasua katika utoaji wa michango ili ziweze kuchangia kama ambavyo nchi zingine zinafanya.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha katika vikao vya bunge hilo vinavyoendelea katika makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki,Mbunge wa EALA nchini Tanzania,James Ole Millya amesema kuwa, nchi kama Tanzania,Kenya na Uganda wanachangia kwa asilimia mia moja ila kuna nchi ambazo michango yake inasuasua hali ambayo inachangia kukwama kwa shughuli za maendeleo katika maeneo hayo.
Millya amesema kuwa, ni vizuri wakuu wa nchi wa jumuiya hizo wakakaa pamoja na kuweza kuzisukuma nchi hizo ili ziweze kutoa michango hiyo kwa wakati na kuharakisha maendeleo katika nchi hizo .
“Leo bajeti imesomwa hapa bungeni ambayo ni Dola milioni 112.9 na bajeti hii inatia matumaini ila hofu kubwa Sisi kama wabunge tunaonea huruma nchi zinazochanga kwa asilimia mia moja kama Tanzania,Kenya na Uganda wakati kuna nchi hazichangii kabisa na tumewakaribisha kwenye jumuiya kwa lengo la kuendeleza mtengamano sasa tunawaomba wasije wakasimamisha jumuiya nafahamu kama nchi hatufanani kiuchumi kwa mazingira ya maendeleo lakini wajitahidi kutoa michango yao kwa wakati ili tuweze kwenda sawa.”amesema Millya.
Amesema kuwa, asilimia 61 ya bajeti iliyosomwa inapaswa kuchangiwa na nchi wanachama lakini mpaka leo wanaochangia kwa asilimia mia ni wadau wa maendeleo na Mashirika mbalimbali .
Aidha ameomba viongozi wakuu wa nchi zetu wasaidie kusukumana huko juu ili watu wote wachangie ili kufikia nyonzi ya kweli na kufikia malengo waliyojiwekea wasaidie kusukumana huko juu ili na wenzetu wachangie.
Naye Mbunge mwingine kutoka Tanzania Dk.Abdullah Makame amesema bajeti iliyosomwa ni ndogo bado haikidhi majukumu ya mtengamano kwani majukumu yameongezeka na jumuiya imepanuka hivyo kunahitajika bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele mbalimbali.
“Hatutegemei mabadiliko yoyote kiutendaji kwani bajeti hii ni ndogo kulingana na majukumu ya mtengamano yaliyopo na majukumu ya mtengamano yameongezeka hatutengemii kwa bajeti hii kitakuwa na mabadiliko yoyote ya kiutendaji”amesema Dk. Makame .
Aidha ameongeza changamoto iliyopo ni kuwa bado nchi zetu hazijaweka vipaumbele vya kutosha katika swala hilo jambo ambalo inapelekea bajeti kuwa ndogo .
Amesema kuwa ,Marais wa nchi hizo walielekeza mawaziri wa nchi hizo kukaa pamoja na kupitia na kuangalia changamoto zilizopo katika nchi hizo na kufanya mapendekezo yao,hivyo nafikiri mawaziri hao wakishakaa watakuja na suluhisho kamili na kuweza kuinasua hali hiyo.