Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa akizungumza katika Kongamano la 12 la Kisayansi lililoandaliwa na MUHAS katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam leo Juni 27, 2024.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha MUHAS Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika kongamano hilo.
…………………..
Na John Bukuku Mloganzila
MUHAS kupitia msaada kutoka serikalini, washirika wa maendeleo na kwa mapato yake ya ndani imeendelea kukuza na kupanua mazingira ya ufundishaji na utafiti huku ikichukua nafasi kubwa katika kutoa ushauri wa kitaalam kwa serikali yetu, mashirika yasiyo ya kiserikali na jumuiya ya kimataifa.
Hayo yameelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa wakati akizungumza kwenye Kongamano la 12 la Kisayansi la MUHAS lililofanyika leo Juni 27, 2024 katika Hospitali ya Muhimbili Mloganzila nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam
Profesa Kamuhabwa ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msaada mkubwa wanaoutoa kwa MUHAS, ambao umeiwezesha taasisi hii kutekeleza majukumu yake.
“Ni kwa msaada huo MUHAS imeendelea kung’ara kitaifa na kimataifa. Tunashukuru sana, ” Amesema Profesa Kamuhabwa.
Leo ni siku ambayo tumeweza kuwaleta pamoja watafiti wa afya nchini na kwingineko na kutafakari maendeleo tuliyofikia kupitia tafiti katika kupunguza changamoto za kiafya katika jamii yetu na kujadili njia ya kusonga mbele.
Amesema Makongamano hayo ya kisayansi yana lengo la kusambaza matokeo ya tafiti za afya nchini na hivyo basi, ni wakati wa kutafakari mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia tafiti hizi kwa ajili ya kuboresha jamii yetu.
Pili kwa sababu, Kongamano la mwaka huu pia ni la kumuenzi Mkuu wetu wa Chuo wa Kwanza na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt Ali Hassan Mwinyi.
Ameongeza kuwa Hayati, Dkt Mwinyi aliteuliwa kuwa Mkuu wa kwanza wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) mnamo tarehe 11 Septemba, 2007, mara baada ya Chuo kupata hadhi ya kuwa Chuo Kikuu Kamili.
“Alikitumikia Chuo hiki katika vipindi vitatu mfululizo mpaka alipoaga dunia tarehe 29 Februari 2024. Katika miaka 17 alipokuwa Mkuu wa Chuo, Chuo kilinufaika moja kwa moja kwa mchango wake katika upanuaji wa miundombinu ya kufundishia, kutoa huduma na tafiti, ikiwemo Kampasi hii mpya ya Mloganzila, hivyo hatuna budi kumuenzi. ” Amesema Profesa Kamuhabwa
Amesema Chuo cha MUHAS kilianza mwaka 1963 kama Shule ya Tiba ya Dar es Salaam. Katika kipindi cha takribani miaka 60, Chuo kimekua katika maeneo yote ikiwa ni pamoja na ongezeko la udahili wa wanafunzi, programu za shahada ya kwanza na za uzamili, tafiti na machapisho katika majarida ya ndani na nje ya nchi.
“Tukiwa Chuo Kikuu kikongwe zaidi cha Afya na Sayansi Shirikishi nchini Tanzania, tunajivunia maendeleo yaliyofikiwa hasa katika nyanja ya mafunzo na tafiti, ” Kamuhabwa
Ametanabaisha kuwa kwa miaka yote MUHAS imeendelea kuwa kitovu cha kutegemewa cha kitaifa kwa matokeo ya tafiti za afya, kusaidia sera na miongozo, na kusaidia taasisi nyingine nchini.
Amesema mpaka sasa Hadi, Chuo kina miradi ya utafiti inayofadhiliwa 150, kinafanya kazi na zaidi ya taasisi 100 za ndani ya nchi na kimataifa, na kuzalisha kati ya machapisho ya kisayansi 450 na 500 katika majarida yenye hadhi ndani na kimataifa kila mwaka.
Profesa Kamuhabwa amesema MUHAS inaendelea kukua na kupanua mazingira ya kufundishia na utafiti, Utekelezaji wa ndoto ya kuwa na vituo vya umahiri katika maeneo mbalimbali ya umuhimu wa kimataifa na wa ndani unaanza kuchukua sura.
Akizungumzia kuhusu awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kituo cha Afrika Mashariki cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu (Centre of Excellence in Cardiovascular Sciences (CoECVS)) Mloganzila amesema uje zi huo huoumekamilika, na kama tunavyoona leo hii tumeanza kufaidika na matunda ya jengo hili.
Mipango ya kuanzisha hospitali ya moyo katika Kampasi hii kama ya awamu ya pili ya CoECVS tayari imeanza.
Aidha mapendekezo ya kuanzisha Kituo cha Afrika Mashariki cha Afya ya Kinywa na Meno hapa katika Kampasi ya Mloganzila yametolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwenye Baraza la Mawaziri wa Kisekta wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hivyo matumaini yetu ni kwamba kutokana na wataalamu tulionao wa afya ya kinywa na meno pamoja na vifaa vya kisasa, Kituo hiki kitaanzishwa MUHAS katika Kampasi hii ya Mloganzila.
Ametoa ombi kwa serikali wamba miradi ya kimkakati kwa nchi katika sekta ya Elimu ya Juu na Afya ipanuliwe zaidi ili kuwezesha kuanzishwa kwa vituo vingi vya umahiri katika kampasi ya Mloganzila.
Amesema kuwa muelekeo wa magonjwa hapa nchini na duniani umekuwa ukibadilika kwa jinsi muda unavyokwenda. miaka ya nyuma, mapambano makubwa yalikuwa ni dhidi ya magonjwa yanayoambukiza lakini kwa sasa changamoto kubwa ni kwenye magonjwa yasiyoambukiza. Ukiangalia pia magonjwa yanayowakabili watoto ni tofauti na magonjwa yanayowakabili watu wazima.
Nchini Tanzania vile vile tunashuhudia mabadiliko ya aina ya magonjwa, ongezeko la idadi ya wazee wanaohitaji huduma za afya, ajali, usugu wa vijidudu vya magonjwa dhidi ya madawa, magonjwa ya afya ya akili na magonjwa yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Magonjwa yote haya yanaendelea kutuathiri kwa kiasi kikubwa na wakati huo huo hali za wananchi na mazingira pia yamebadilika. Hivyo basi, ni muhimu kujiuliza nafasi ya sayansi katika kukabiliana na changamoto hizi. Na hili ndilo lengo hasa la Kongamano la mwaka huu, kupitia tafiti mbalimbali tutapata fursa ya kusikia, kujadili na kuja na mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizi. ” Amemaliza Profesa Kamuhabwa
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha MUHAS Dkt. Harrison Mwakyembe amemshukuru Makamu Mkuu wa Chuo hicho na wote waliofanikisha Kongamano hilo, wanataaluma, wanasayansi, wanafunzi na watu wote kwa ujumla kwa kuhudhuria kongamano hilo na kuwatakia majadiliano yenye manufaa makubwa kwa taifa.