*Asema ni chanzo cha mmomonyoko wa maadili
*Ahusisha na ukatili wa kijinsia na mauaji ya Albino
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kuzingatia utamaduni wao na katu wasiendekeze utamaduni wa kigeni kwan kwa kufanya hivyo ni sawa na kuuza uhuru wao kama nchi.
Dkt. Biteko amesema hayo Juni 27, 2024 katika viwanja vya Kisesa, wilayani Magu, Mkoani Mwanza wakati akimwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kufunga tamasha la Utamaduni wa Kisukuma, Bulabo lililoshirikisha watemi kutoka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa na Mkoa wa Tabora.
“Utamaduni wetu unatupa heshima na tamasha kama hili linatuwezesha kama nchi kuzingatia utamaduni wetu na kuwawezesha Watanzania kujitambua, kitendo cha kuiga utamaduni wa nchi nyingine bila kupima madhara unaweza kutuharibia na kuondoa heshima yetu”
Aliongeza kuwa “Vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinavyoendelea katika maeneo mbalimbali nchini havina mizizi katika utamaduni wa Watanzania na jamii za kiafrika, hivi sasa tunashuhudia vitendo kama mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), Mapenzi ya jinsia moja na Unyanyasaji wa kijinsia ni baadhi ya mambo yanayotokana na vitendo vya kuiga kutoka maeneo mengine”.
Aidha, Dkt. Biteko amesema utambuzi wa makabila miongoni mwa Watanzania ni kwa ajili ya kutaniana na sio kwa ajili ya kubaguana miongoni mwao kutokana na Utamaduni wa Watanzania kuishi kama familia moja na hivyo amehimiza kufanyika kwa matamasha mengi ya utamaduni ili kuenzi mila na kudumisha utamaduni wa Mtanzania.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka Watanzania kujipanga vema kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025, “Chagueni viongozi wenye uwezo wa kuwaongoza na kuwaletea maendeleo hata kama hawana fedha na katu msiingie kwenye mtego wa kuchagua viongozi wasio na uwezo kwa kigezo cha fedha” alilisitiza Dkt. Biteko.
Awali, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali kupitia wizara kwa kushirikiana na watemi wa maeneo mbalimbali imepanga kufanya tamasha kubwa zaidi litakalofanyika katika Viwanja vya Majimaji, Songea Mkoani Ruvuma.
Naye, Kiongozi wa Umoja wa Watemi nchini Anthoni, Ameishukuru Serikali kwa kuwatambua na kuwawekea mazingira rafiki katika kuendeleza matamasha ambayo yanaendeleza mila na desturi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu, Tamasha la Utamaduni wa Wasukuma limeshirikisha watemi kutoka mikoa saba ambayo ni Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Tabora.