KATIKA kuendana na mabadiliko ya Teknolojia Benki ya Equity Tanzania imezindua Kampeni ya Hapohapo ambayo inamuwezesha mteja kufungua akanti kwa njia ya kijiditi kwa kutumia simu ya mkononi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika jana katika benki ya Equity tawi la Mbagala, Meneja wa tawi hilo, Salum Halfan alisema kuwa kampeni hiyo itasaidia katika ukuaji wa uchumi kwa kuwa mteja ataweza kuendelea na kazi zake bila kufika benki kupanga foleni.
“Kwa mfano Mfanyabiashra badala ya kuacha biashara yake na kwenda kupanga foleni benki kwa ajili ya kufungua akaunti ataweza kufungua kupitia simu yake huku ajkiendelea kuhudumia wateja wake na bila kupoteza muda katika kuendeleza gurudumu la uchumi” alisema Salum.
Awali akizindua kampeni hiyo Kaimu Mkuu wa kitengo cha Malipo Benki ya Equity Tanzania, Haidari Chamshama alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki kwa kumfikia mteja popote alipo.
Chamshama alisema kuwa huduma hiyo ni salama na suluhu kwa watanzania ambao hawatumii huduma rasmi za kifedha katika kutumana kuhifadhi fedha zao.
Kwa upande wake mteja wa Benki hiyo, Theresia Elias alisema kuwa huduma hiyo itasaidia kuondoa msongamano wa wateja wanaofika benki kwa ajili ya kufungua akaunti na pamoja na mzunguko wa kutafuta viambatanishi mbalimbali kwa ajili ya kufungua akaunti.
Huduma ya Hapohapo inamuwezesha mteja kufungua akaunti popote alipo kwa kutumia simu ya mkononi na kitambulisho cha uraia (NIDA)