Salum Hamduni Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru akifungua semina ya Asasi za Kiraia kuhusu kupiga vita rushwa katika uchaguzi wa serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao wa 2025. Semina hiyo imefanyika leo Juni 26, 2024 kwenye Ofisi za Takukuru Upanga jijini Dar es Salaam
Bi. Neema Mwakalyelye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Salum Hamduni ili kufungua semina hiyo iliyofanyika leo Juni 26, 2024 kwenye Ofisi za Takukuru Upanga jijini Dar es Salaam.
………………
KUELEKEA Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2025 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU,) imekutana na viongozi wa Asasi za Kiraia (AZAKI,) na Asasi zisizo za Kiserikali (AZISE,) kwa lengo la kujadili na kuweka mkakati wa kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua warsha iliyoikutanisha Taasisi hiyo na Asasi hizo; Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP. Salum Rashid Hamduni amesema TAKUKURU inatambua mchango wa wadau hao katika mapambano dhidi ya rushwa.
“Vitendo vya Rushwa katika uchaguzi vinasababisha kuwa na uchaguzi usiozingatia misingi ya haki na usawa na hili limekuwa tatizo la kidunia ambapo hata Tanzania haijaachwa salama….Tatizo hili limeifanya TAKUKURU kuendelea kubuni mikakati ya kuikabili rushwa katika uchaguzi kwa kuwa madhara yake ni makubwa sana.” Amesema.
Akieleza madhara ya rushwa wakati wa uchaguzi CP. Hamduni ameeleza ni pamoja na upatikanaji wa viongozi wasio waadilifu, wanaojihusisha na vitendo vya Rushwa pamoja na kutozingatia misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo mambo ambayo ni muhimu katika ustawi wa wananchi.” Amesema.
“La kusikitisha zaidi Rushwa wakati wa uchaguzi hudhalilisha utu kwa kufananisha thamani ya mtu na hongo anayopewa ili apige au asipige kura pia rushwa wakati wa uchaguzi husababisha uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya kisiasa, kusababisha Taifa kuendelea kugubikwa na rushwa, wananchi kutokuwa na imani na Serikali pamoja na kudhoofisha utawala bora na demokrasia kwa wananchi wenye sifa za uongozi bora kushindwa kugombea au kutoteuliwa kwa kutokuwa tayari kutoa hongo.” Amesema.
Aidha amesema, Kutokana na athari zinazoweza kusababishwa na Rushwa katika Uchaguzi TAKUKURU imeona ni busara kukutana na viongozi hao wa kwa lengo la kujadili tatizo la rushwa katika uchaguzi, madhara yake na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia na kupambana na Rushwa kabla madhara hayajatokea.
“TAKUKURU pekee haiwezi kutekeleza jukumu hili la Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Tunatambua kuwa Asasi za Kiraia zimekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki na usawa pamoja na kuhamasisha wananchi kutambua wajibu wao katika masuala mbalimbali ya kijamii, uchumi na siasa ikiwemo kushiriki uchaguzi na shughuli za maendeleo…Kwa ukaribu wenu na jamii tunaamini mchango wenu katika kuandaa mkakati wa kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi.” Amesema.
CP. Hamduni amesema mkakati huo wa kudhibiti vitendo vya Rushwa kwenye uchaguzi utakuwa na faida kubwa kwa Taifa ikiwemo kuchaguliwa kwa viongozi bora watakaoongoza kwa mujibu wa sheria na kutekeleza mipango ya maendeleo.
“Warsha hii muendelezo wa jitihada za Serikali za kudhibiti Rushwa katika uchaguzi ambapo Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassaen imeanza na inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki usiogubikwa na vitendo vya Rushwa. Na hatua hizo ni pamoja na kuanzisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC,) kutunga sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani 2024 pamoja na kuiwezesha zaidi TAKUKURU kwa kushirikiana na wadau wengine ili iweze kuzuia na kupambana na Rushwa katika Uchaguzi na Warsha hii ni sehemu ya uwezeshaji huo.” Ameeleza CP. Hamduni.
Vilevile amefafanua kuwa TAKUKURU haipo nyuma kwa kuzingatia sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura 329 imejizatiti kikamilifu kuzuia na kupambana na Rushwa nchini ikiwemo katika uchaguzi kwa kuelimisha Umma kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi, kuchukua hatua za haraka za kudhibiti vitendo vya rushwa, kushirikiana na wadau mbalimbali na kuhamasisha wananchi kutojihusisha na rushwa ikiwemo katika uchaguzi pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kufanya uchunguzi na kuendesha mashtaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO,) Dkt.Lilian Badi amesema TAKUKURU imekuwa ikishirikiana na Asasi za kiraia katika mapambano ya rushwa na kueleza kuwa kuelekea wakati wa uchaguzi ni vyema Asasi hizo zikapewa vibali ili ziweze kutoa elimu kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ili kuleta matokeo chanya dhidi ya mapambano ya rushwa.
Dkt. Lilian amesema ushirikishwaji wa wadau hao ni muhimu kwa kuwa Asasi za Kiraia huwafikia wananchi katika ngazi zote na kuwahudumia katika sekta mbalimbali hivyo kupitia mitandao na majukwaa elimu na hamasa ya kuepuka vitendo vya rushwa itawafikia wananchi kwa kiasi kikubwa.
Lilian Liundi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) amesema mtandao huo umekuwa ukipigania nafasi za ushiriki wa wanawake katika uongozi na kupitia warsha hiyo watajadili vikwazo na kuona namna ya kutoa elimu na kuripoti changamoto katika uchaguzi ikiwemo rushwa ya ngono kwa wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi.