Na Sophia Kingimali
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Soko la Kimataifa la Kariakoo Martin Mbwana ametoa rai kwa wafanyabiashara kufungua maduka yao na kuendelea kufanyakazi zao wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kutatua madai yao.
Rai hiyo ameitoa leo juni 26,2024 sokoni hapo wakati akiongea na wafanyabiashara wa soko hilo kuhusu maazimio waliyoyafikia na serikali katika kikao chao kilichofanyika Dodoma.
Amesema serikali imeahidi kushughulikia changamoto zao ambapo kwa kuanza TRA imeridhia kutokufika katika soko hilo na kukamata kamata mpaka hapo watakaposhughulikia mifumo yao.
Amesema pamoja na TRA kusitisha kamatakamata pia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka TRA kuboresha mfumo wa forodha bandarini ambapo mpaka kufikia Agosti 8 mfumo uwe umesharekebishwa.
“Nikiwa kama muwakilishi wenu wafanyabiashara niwaombe mfungue biashara zenu kwa hiyari muendelee kufanyabiashara kwani serikali imeridhia madai yetu na imeahidi kushughulikia hatulazumishi mtu kufungua maana kufunga na kufungua ni utashi wa mtu mwenyewe”,Amesema Mbwana.
Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo amewataka polisi kutokutumia nguvu kwa wafanyabiashara kwani kufunga na kufungua ni wajibu wa mfanyabiashara mwenyewe.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wameridhia kufungua maduka yao huku wengine wakiendelea na mgomo huo huku wakiihitaji Rais kufika sokoni hapo na kuwasikiliza.