Mkurugenzi wa maswala ya afya katika kampuni hiyo,Dk .Hussein Abradha akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
……………..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .Kampuni ya uokoaji ya KiliMedAir Aviation iliyopo mkoani Kilimanjaro imeanzisha huduma ya uokoaji wa haraka kwa njia ya helikopta ili kuweza kuokoa muda na kufika eneo la tukio haraka kabla madhara yoyote hayajatokea.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa maswala ya afya katika kampuni hiyo,Dk .Hussein Abradha wakati akizungumza kwenye kambi ya madaktari bingwa wanaotoa huduma za matibabu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo mkoani Arusha .
“Sisi tumeshiriki katika kambi hii lengo la kutoa elimu kwa wadau na wananchi ili waweze kuelewa kampuni yetu na ufahamu shughuli tunazofanya katika kuwahudumia wananchi kwa wakati na kuokoa muda kwa kutumia helikopta “amesema.
Dk.Hussein amesema kuwa,kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma ya uokoaji kwa watu waliopata dharura katika maeneo mbalimbali ikiwemo hifadhi na hata maporini kwani helikopta hiyo ina uwezo wa kupenya popote kwa wakati na muda muafaka .
Amesema kuwa,wamekuwa wakitoa huduma hiyo ndani ya hifadhi ya Tanapa kwa kuwahudumia watalii na hata wageni mbalimbali wanaopatwa na changamoto zozote wanapokuwa maeneo ya hifadhi na hata mlimani ambapo wamekuwa wakifika kwa wakati kwa ajili ya kuwawahisha kupata huduma ya haraka sehemu husika.
“ndani ya helikopta hiyo kunakuwepo na daktari kwa ajili ya kutoa huduma ya kwanza pindi wanapomkuta mteja kapata changamoto yoyote kabla ya kumwahisha hospitali kupata huduma zingine na tumejikita zaidi kwenye maeneo ya porini milimani pamoja na mbugani katika kuhudumia wageni pamoja na watalii wa nje “amesema Dk.Hussein.
Ameongeza kuwa, ambulance hiyo ya helikopta imekuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa wanaokumbana na changamoto mbalimbali wakiwa maeneo ya hifadhi,porini na hata mbugani kwani ina uwezo wa kutua popote .
Amesema kuwa, mbali na huduma hiyo wamekuwa wakitoa huduma zingine za anga ikiwemo za kukodishwa kwa ajili ya kuhudumia watalii kulingana na mahitaji ya mteja anavyotaka.
Aidha ametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo hospitali mbalimbali kuitumia kampuni hiyo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za haraka na kwa muda muafaka .
Nao baadhi ya wananchi ,Selina Mohamed wamepongeza utoaji wa huduma hiyo ya matibabu kwani inaleta manufaa makubwa sana kwao na kuokoa gharama badala ya kwenda kufuata huduma hiyo mbali wanaweza kuipata hapa hapa kwa haraka na muda muafaka .
“Tunaomba muda zaidi uongezwe kwani wiki moja haitoshi kabisa kutokana na kuwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo ni wengi na hivyo wiki moja haitoshi kabisa kuwafikia wananchi wote.”wamesema wananchi hao.