MKOA wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache nchini ambayo imebarikiwa na Mwenyezi Mungu kuwa na vivutio vya aina zote za utalii,ambavyo ni utalii wa ikolojia na utamaduni.
Mkoa wa Ruvuma una mapori manne ya wanyamapori ambayo ni sehemu ya mfumo wa Selous.Mapori hayo ni Selous ambalo hivi sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere lenye ukubwa wa kilometa za mraba 50,000,Pori la Liparamba lenye kilometa za mraba 571,Gesimasoa lenye kilometa za mraba 764 na Litumbandyosi lenye kilometa za mraba 464.
Hata hivyo utafiti umebaini bado kuna vivutio vingi ambavyo havijaibuliwa na kutambuliwa ili kutoa fursa za uwekezaji kwa watalii toka ndani na nje ya nchi.
Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema vivutio hivyo vikiendelezwa vinaweza kuchangia pato la Taifa na kuinua uchumi wa wananchi na kwamba kinachotakiwa ni kuboresha Zaidi miundombinu ya barabara na hoteli za kitalii ili kuvutia watalii kuvifikia vivutio hivyo.
Hatua mbalimbali zinachukuliwa na serikali kuhakikisha miundombinu mbalimbali inaboreshwa katika Mkoa wa Ruvuma ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ambapo hivi sasa wawekezaji wameanza kuonesha nia ya kuwekeza katika Mkoa wa Ruvuma.
Pia serikali imetoa mwongozo wa uwekezaji wa Mkoa wa Ruvuma ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa mwaka 2019. Mwongozo huo unapatikana kwenye tovuti ya Mkoa wa Ruvuma ambayo ni www.ruvuma.go.tz
Utafiti umebaini karibu kila wilaya iliyopo katika Mkoa wa Ruvuma ina vivutio mbalimbali vya utalii vinavyoweza kufungua milango ya utalii katika wilaya husika na kutoa ajira kwa vijana kupitia sekta hiyo adimu hapa nchini na duniani kote.
Vivutio vinavyoubeba Mkoa wa Ruvuma ni ziwa Nyasa,Mto Ruvuma,Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Hifadhi ya mazingira asilia ya Mwambesi,Bustani ya asili ya Luhira na ushoroba wa Selous-Niassa.