Wavuvi wakiendelea kuchambua nyavu zao ndani ya mtumbwi kwenye fukwe ya Ziwa Nyasa iliyopo katika kijiji cha Ikombe, Kata ya Matema wilayani Kyela. Mitumbwi kama hii pia ndiyo hutumika kusafirishia wagonjwa na wajawazito kutoka Kijiji cha Ikombe kwenda Kituo cha Afya kilichopo Matema hatua ambayo huatarisha maisha yao hasa ziwa hilo linapokuwa na dhoruba kali.(Picha na Joachim Nyambo)
……………
Na Joachim Nyambo.
*Ukosefu wa Barabara unavyochangia vifo vya wajawazito, watoto wachanga kijijini Ikombe
1976 ndiyo Mwaka kilipoanzishwa Kijiji cha Ikombe kilichopo katika Kata ya Matema wilayani Kyela Mkoani Mbeya. Shughuli kubwa ya wakazi wa kijiji hiki ni uvuvi hasa wa samaki na dagaa, kilimo pamoja na ufinyanzi wa zana mbalimbali zitokanazo na udongo ikiwemo vyungu.
Wajawazito kujifungulia majumbani au wakiwa safarini ni sehemu ya changamoto zinazowakabili wakazi wa kijiji hiki kwa miaka yote waliyoishi hapa. Ni kijiji kilicho pembezoni mwa Ziwa Nyasa kikiwa kwenye safu za milima ya Livingstone.
Kukosekana kwa barabara ndiyo sababu kubwa ya wagonjwa na wajawazito kutozifikia huduma stahiki kwa wakati. Wakazi wanategemea kupata huduma za matibabu katika Kituo cha Afya kilichopo Matema yalipo makao makuu ya kata. Ni umbali wa kilometa saba kutoka kijijini hapa.
Wakazi hao wanasema kwa kukosa barabara usafiri wao mkuu ni wa njia ya maji ambapo hutumia boti ndogo au mitumbwi ya kusukumwa kwa kasia kusafirisha wagonjwa na wajawazito kutoka kijijini hapa kuwapeleka Matema kama wanavyofanya pia wanaposafirisha bidhaa za kilimo, uvuvi na ufinyanzi kuzipeleka sokoni.
Wanasema changamoto inayopelekea wajawazito kujikuta wakijifungulia majumbani na kuhatarisha maisha yao na watoto wachanga wanaozaliwa ni pale ziwa linapokuwa limechafuka na kugubikwa na dhoruba. Hapo hakuna namna inabidi wasubiri hadi hali za pepo za ziwa ziwe shwari jambo ambalo uchungu wa mjamzito hauwezi kulisubiri.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Ikombe, Happiness Ambanisye anasema wapo wajawazito wanaopoteza maisha kwa kushindwa kusafirishwa kwenda Matema ziwa linapokuwa na dhoruba kali. Hii hutokea pia kwa watoto wachanga wanaozaliwa hasa wanaokuwa wanahitaji huduma saidizi wasizoweza kuzipata kutoka kwa wakunga wa jadi waliopo kijiji hapo.
“Ziwa likichafuka hakuna namna nyingine ya kumsafirisha mjamzito anayekaribia kujifungua. Hakuna usafiri wa gari kwakuwa hakuna barabara na tumezingirwa na milima ambayo hata pikipiki haiwezi kutumika.”
Anasema kuna wakati pia inapobidi wakazi hulazimika kuwabeba kwa machela wajawazito ili waweze kutumia njia za porini zilizopo milimani jambo ambalo huongeza hatari kwao au wagonjwa mahututi.
“Ukweli ni kuwa sisi wanawake ambao bado tuko kwenye umri wa kuzaa tunaishi kwa hofu kubwa hapa kijijini. Ziwa likichafuka namna nyingine ya kukusaidia labda wakubebe kwa machela kupita njia za milimani. Sasa umbali wa kilometa saba wanapambana na mawe makubwa na kupita eneo la milima ni hatari zaidi.”
“Hizo njia za huko mlimani siyo rafiki kabisa kwa mgonjwa hasa mjamzito. Anajikuta anaongezewa maumivu zaidi pale wanapotumia njia hiyo kumsafirisha.”
Mkazi mwingine Vanessa Nkudu anasema changamoto ya usafiri kwenye eneo la uzazi haliathiri wakati wa kujifungua pekee bali pia mwenendo mzima wa uangalizi wa kihuduma za afya za mtoto anapokuwa tumboni na hata anapozaliwa. Wajawazito wanashindwa kuhudhuria kliniki kwa wakati kwa tarehe walizopangiwa na pia kuwapeleka watoto waliozaliwa pale ziwa linapokuwa na dhoruba.
“Sote tunatambua kuna tarehe ambazo mjamzito hupangiwa kwenda kliniki kwaajili ya kuchunguzwa na kupewa ushauri na wataalamu wa afya juu ya mwenendo wa ujauzito wake. Lakini pia hata anapokuwa amejifungua bado anapangiwa siku za kumrudisha mtoto kliniki.”
“Na miongoni mwa vitu anavyotakiwa kuzingatia mama mjamzito au aliyejifungua ni pamoja na tarehe anazopaswa kupata chanje zake au za mtoto sasa inapotokea siku hiyo ziwa limechafuka ina maana hawezi kufuata huduma hiyo. Na kuna wakati hali ya ziwa inakuwa mbaya si siku moja pekee inaweza kuchukua mud mrefu.” Aliongeza.
Diwani wa Kata ya Matema, Antony Peter anakiri kutokea kwa vifo vya wajawazito 11 vilivyotokana na kukosekana kwa usafiri kijijini hapo. Ni hatua anayosema inaleta majonzi kwa kila mkazi kila wanapokumbuka matukio ya vifo vyao. Wapo waliokufa na watoto wao na wapo walioacha watoto wachanga wakaishi bila mama zao.
“Ni kweli hao akina mamam kumi na moja wanaowasema walipoteza uhai je familia zao tuwalipe nini. Ni jambo linasikitisha sana.” Anasema Peter.
Ombi kuu la wakazi wa kijiji hiki na kata ya Mtema kwa ujumla ni serikali kukamilisha ujenzi wa barabara kutoka kijiji cha Matema hadi kijijini kwao ili na wao waweze kufaidi matunda ya uhuru wa taifa lao.
“Barabara kutoka Matema Liulilo mpaka hapa ni kilometa saba tu …nina hakika barabara inaweza kufika Ikombe. Mbona mwaka 1976 alifika rais wa Zanzibar hapa kwenye kiwanda cha kukiwa na kiwanda cha ufinyanzi kwa nini barabara inashindwa kufika Ikombe!”
Mbunge wa jimbo la Kyela Ally Mlaghila anasema tayari serikali imeshatenga fedha kwaajili ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita saba.
“Rais Samia Suluhu Hassan amekwisharuhusu na kusema ni wakati sahihi kwa wakazi wa kijiji cha Ikombe wapate barabara ili wawe na njia mbadala inapotokea matatizo ndani ya ziwa waweze kusafiri kufuata mahitaji muhimu ikiwemo ya kiafya.”
Mlaghila aliyasema hayo wakati wa zoezi la kufunga kambi ya Mafunzo kwa vijana wa Umoja wa Cchama Cha Mapinduzi UVCCM kwenye Kata ya Matema.