Naibu Waiziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Mhe. Dkt. Festo Dugange (Mb) amesema serikali kupitia sera ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI ilikwisha elekeza kwamba Huduma za Afya kwa kinamama Wajawazito zinazohusu kujifungua na Watoto chini ya Miaka mitano zinatolewa bila malipo yoyote.
Mhe. Dkt. Dugange amesema hayo katika kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Azan Mwinyi aliyetaka kujua je serikali inatoa kauli gani juu ya baadhi ya hospitali zinazodai wakinamama watoe hela kwaajili ya vifaa wapoenda kujifungua?
“Nikweli kwamba kumekuwa na changamoto kwa Baadhi ya vituo vya huduma za afya kutoza gharama za vifaa kwa wajawazito wanapofika kupata huduma ya mama na mtoto na serikali kupitia sera ya wizara ya afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI ilikwisha elekeza kwamba Huduma za afya kwa kinamama Wajawazito zinazohusu kujifungua na Watoto chini ya Miaka mitano zinatolewa bure”
Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri kote Nchini na Waganga Wakuu kwa kushirikiana na Waganga Wafawidhi wanatakiwa kuhakikisha wanasimamia Sera hiyo kwa kuwa na vifaa Tiba vyote vinavyohitajika kwaajili ya kina mama wajawazito na Watoto chini ya miaka mitano.
Akijibu swali la msingi la Mhe. Maryam Azan Mwinyi, mbunge wa viti maalum, aliyeuliza Je, ni lini Serikali itaweka vifaa tiba katika majengo ya Huduma za Mama na Mtoto katika Halmashauri mbalimbali nchini? Dkt. Dugange amesema
“Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri. Katika kipindi cha mwaka 2022/23 hadi 2023/24, jumla ya shilingi bilioni 186.3 zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vikiwemo vifaa vya huduma ya mama na mtoto”.