Na. WAF – Dodoma
Kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya kisasa ye jeshi iliyopo Msalato Jijini Dodoma inayotarajiwa kuwa ya Level 4 utasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na Hospitali ya Benjamin mkapa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Tarehe 25 Juni, 2024 alipotembelea Ujenzi wa Hospitali hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kuhudumia wagonjwa Januari 2025.
“Uwepo wa Hospitali hii tunaaamini itasaidia katika kuboresha sekta ya afya kwani itawezesha wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani kupata huduma bora na za kibingwa ambazo zitasaidia kuzipunguzia mzigo mkubwa Hospitali nyingine zilizopo Dodoma”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameongeza kuwa kumeanza kutokea changamoto katika hospitali ya Rufaa ya mkoa na hospitali ya Benjamini Mkapa kuanza kujaa wagonjwa hivyo amelipongeza jeshi kwa kujenga Hospitali hiyo kubwa na nzuri kwa ili iweze kusaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa.
Pia Waziri Ummy amewapongeze wanajeshi wa jeshi la wananchi wa Tanzania Kwa kuchangia kutoa huduma za matibabu katika maeneo mbali mbali nchini.
“Nashukuru kwa sera yenu ya kutoa huduma matibabu kwa Raia na sio tu wanajeshi kwani raia wana imani kubwa sana na huduma za matibabu zinazotolewa katika hospitali za jeshi”. Amesema.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Jeshi la wananchi kuona ujenzi wa hospitali hiyo unafika mwisho na kuanza kutoa huduma zinazotarajiwa.
“Sisi kama Wizara tutahakikisha tunashirikiana ile azma ya kuwa hospitali ya jeshi Level 4 isiwe tu majengo bali kwa vifaa na wataalamu ili kusaidia iweze kutoa huduma kama sekta tunacyotaka”. Amesema.