NA VICTOR MAKINDA. IGUNGA TABORA.
Katika hatua ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ya kuambukizwa yanayotokana na kusambaa kwa taka na maji taka, Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira mjini Igunga, IGUWASA inatarajia kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kutibu maji taka mwezi Oktoba mwaka huu.
Akitoa taarifa mbele ya kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Igunga,mkoani Tabora, Mkurugenzi Mtendaji wa IGUWASA, Mhandisi Humphrey Mwiyombela alisema kuwa, ujenzi wa mtambo huo ulianza mwezi Julai 2023 na unatarajia kukamilika octoba mwaka huu.
“Pamoja na jukumu la kusambaza maji safi na salama ya kunywa mjini Igunga, IGUWASA tuna jukumu jingine la kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa safi.” Anasema Mwiyombela.
Mwiyombela anasema kuwa katika kuhakikisha mji wa Igunga unakuwa safi, mamlaka hiyo inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji taka unaogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 fedha kutoka serikalini.
Anaongeza kuwa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 23 ambapo kukamilika kwake kutawanufaisha jumla ya wakazi 82768 wa mji wa Igunga na vitongoji vyake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Igunga, Mafunda Temanya anasema kuwa mradi huo ni muhimu kwa ustwi wa afya za wananchi wa Igunga, hivyo aliwataka IGUWASA kuhakikisha wanamsimamia mkandaraji vizuri atekeleze mradi kwa wakati.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Igunga, Ebenezer Ole Mainoya, amesema kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM inasisitiza serikali kapambana na maradhi hivyo miradi ya usafi wa mazingir ina mchango mkubwa katika kuboresha afya za wananchi.