Mkuu wa wilaya ya Arumeru akipata maelezo katika moja ya banda linalouza viautilifu mbalimbali
Meneja masoko wa kampuni ya Suba Agro, Rizwan Velji akizungumza katika mkutano huo mkoani Arusha.
………………
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini TPHPA imeweka mikakati ya msingi inayolenga kuzalishwa mazao yasiyo na sumu ili kupanua wigo katika soko la dunia kwa mustakabali wa kulinda afya za walaji.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa Wadau wa TPHPA Jijini Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyetarajiwa kuwa Mgeni Rasmi, ameipongeza mamlaka hiyo kwa jitihada zake kubwa za kuleta mabadiliko na uzalishaji wenye tija katika sekta ya kilimo.
Aidha ameongeza kuwa, Sekta ya Kilimo ni mkombozi kwani inategemewa kuongeza ajira kwa jamii hususani vijana na wanawake, kuimarisha mfumo wa chakula na kuongeza pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
“Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta hii muhimu imeongeza bajeti kutoka Bilioni 970 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kufikia Tirioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, hii yote ni kuhakikisha tunajiimarisha katika soko la dunia na kuzidi kuwa bora katika uzalishaji wa chakula cha kutosha”
“Nawasisitiza Mamlaka ya TPHPA kuhifadhi mbegu za asili, hii itasaidia kuepuka upotevu wa mbegu bora zinazotegemewa katika ushindani wa soko la dunia” amesisitiza Kaganda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPHPA Prof. Andrew Temu amesema kuna muelekeo wa mamlaka hiyo kutimiza malengo yake ya kuboresha afya za watu kutokana na juhudi na mikakati mbambali inayowekwa.
Ameongeza kuwa, TPHPA inatambua juhudi za serikali katika utekelezaji wa majukumu yao, ushauri na maelekezo muhimu yenye lengo la kuhakikisha mamlaka hiyo inaimarika na kuendelea kufanya vizuri.
“Tunaendelea na jitihada za kutanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji lakini pia kupambana na changamoto mbalimbali zikiwemo usugu wa viuatilifu, kupotea kwa vinasaba katika mimea ya asili, ubunifu na mbinu juu ya viuatilifu sambamba na hayo tunajipanga kwa matumizi ya akili mnemba ili kuendana na Maendeleo ya Teknolojia lakini pia kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi” ameeleza Prof. Temu.
Mkurugenzi wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru ameeleza kuwa, mkutano huu umetoa fursa kwa wadau wa sekta ya kilimo kubadilishana uzoefu, changamoto na ushauri katika kuleta mageuzi kwa sekta hiyo.
Naishukuru kamati ya kudumu ya Bunge, inayosimamia Wizara ya Kilimo, Viwanda na Biashara kwa kupitisha bajeti ambayo imetupa tumaini la kufikia malengo tuliyojiwekea TPHPA” ameeleza Prof. Ndunguru.
Kwa upande wa wadau waliodhuria katika mkutano huo,Meneja masoko wa kampuni ya Suba Agro,Rizwan Velji amesema kuwa,amesema kuwa uwepo wa mkutano huo ni fursa pekee ya kuweza kuwaunganisha na kuwa karibu na wakulima na kuweza kutoa elimu kwao kuhusu mbegu bora zinazovulimia ukame.
Rizwan amesema kuwa ,kampuni hiyo imetoka mbegu aina mbili ambazo zinavumilia ukame na kuweza kupambana na hali yoyote ya hewa na kumwezesha kuweza kupata mazao mengi shambani.
“Sisi hatusambazi mbegu tu bali tunahakikisha timu yetu ya shamba darasa inamfuatilia mkulima kwa karibu tangu anapoanza kupanda hadi kuvuna sambamba na kumpatia elimu juu ya matumizi sahihi ya viatilifu ili waweze kutumia dozi inavyotakiwa.”amesema Rizwan.