Na Mwandishi wetu, Kiteto
MBUNGE wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kiteto fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mbunge Ole Lekaita amesema Kiteto imepokea shilingi 965,280,029 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Ndugu wananchi wenzangu wa Jimbo la Kiteto, nachukua fursa kuwafahamisha kuwa tumepokea fedha shilingi 965,280,029 kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” amesema.
“Nimezungumza na Waziri wa Tamisemi, Mhe. Mohamed Mchengerwa na amethibitisha kuwa pesa zimetumwa na Mkurugenzi wetu CPA Hawa Hassan Abdul amenithibitishia kupokelewa kwa fedha hizo,” amesema Ole Lekaita.
Amesema kuwa fedha hizo zitatumwa katika Kata za Ndirigish na Makame bila kuchelewa na mchanganuo wa fedha hizo ni kama ifuatavyo.
Amesema ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Makame kata ya Makame shilingi 584, 280,029 ujenzi wa mabweni, madarasa na vyoo shule ya sekondari Ndirigish, Kata ya Ndirigish shilingi 381,000,000.
“Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kiteto, tunamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama yetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote Serikalini,” amesema Ole Lekaita.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Samia kuendelea kuboresha maisha yetu wana Kiteto kwa kuendelea kutuletea miradi mikubwa ya maendeleo na kushughulikia changamoto za wananchi katika wilaya yetu na ahadi za CCM zinaendelea kutekelezwa,” amesema Ole Lekaita.
“Ndugu wananchi wenzangu wa Kiteto, tunayo kila sababu ya kutoa shukrani kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Ole Lekaita.
Ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama Samia kwa kuendelea kuwapa fedha nyingi kwa ajili ya kutatua miradi ya maendeleo.
“Tumuombee Mhe. Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan Mwenyezi Mungu ampe afya njema na kumlinda vyema ili aendelee na maono yake mazuri katika kujenga taifa letu,” amesema Ole Lekaita.
Amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kusikia kilio cha wana Kiteto kupitia sauti yake Bungeni.
“Ndugu wananchi wenzangu, kwa dhati kabisa nawahakikishia kuwa nitaendelea kuwa sauti yenu Bungeni na kuwawakilisha ipasavyo kwa unyenyekevu na uaminifu mkubwa,” amesema Ole Lekaita.
Ametoa wito kwa watumishi wote kuhakikisha kuwa miradi hiyo inasimamiwa vizuri na kwa ufanisi mkubwa ili wananchi wapate huduma hizo kwa wakati.
“Kiteto yetu inaendelea kung’ara! Mungu Ibariki Kiteto! Mungu Ibariki Tanzania! Mungu ambariki Mhe. Rais wetu mpendwa Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Ole Lekaita.