Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya, Elukaga Mwalukasa akielezea dhima ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) kwa waandishi wa habari mkoani Mbeya walioshiriki warsha ya mafunzo ya kujenga uelewa juu ya programu hiyo inayotekelezwa nchini kote na serikali kwa kushirikiana na wadau. Semina hiyo iliandaliwa na Shirika la Shalom Development Organizatio kwa ufadhili wa Mtandao wa Maendeleo ya Awali ya Mtoto(Tecden)(Picha na Joachim Nyambo)
Heneliko Malo, Mshindi wa Tuzo ya Habari za Jinsia na watoto upande wa redio kwenye kinyang’anyiro cha mashindano ya Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari(EJAT) Mwaka 2023 zilizondaliwa na Baraza la habari Tanzania (MCT), Heriko Malo akitoa ushuhuda wa namna alivyoanza kupenda kuandika habari za watoto kwa waandishi wa habari mkoani Mbeya walioshiriki warsha ya mafunzo ya kujenga uelewa juu ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM)(Picha na Joachim Nyambo).
……………..
Na Joachim Nyambo
“NILIKUWA nikimfuatilia Bwana Nyambo alipokuwa akifanya habari za watoto wakati ule tukiwa tunaendesha pamoja kipindi cha Amka Bomba pale redioni kwetu. Ni miaka kadhaa sasa imepita na nadhani wakati ule Programu hii ya PJT-MMMAM ilikuwa haijaanza. Walikuwa wakifanya programu ya Mtoto Kwanza nafikiri.”
“Kila alipofanya story ya watoto ilinipa msukumo wa kutaka kujua zaidi uandishi wa habari hizi. Ndiyo sababu hata alipoondoka niliwiwa kuendelea kufanya habari za watoto kwenye kipindi chetu na leo hii najivunia nina tuzo kutoka EJAT”
Anasema Heneliko Malo, mshindi wa Tuzo ya Habari za Jinsia na watoto upande wa redio kwenye kinyang’anyiro cha mashindano ya Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari(EJAT) Mwaka 2023 zilizondaliwa na Baraza la habari Tanzania (MCT). Malo ni mwandishi na mtangazaji wa Kituo cha Redio Bomba FM kilichopo mkoani Mbeya.
Malo alitoa ushuhuda huo alipokuwa mshiriki wa Warsha ya Siku moja ya Mafunzo ya Kuwajengea uelewa waandishi wa habari juu ya Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi , Makuzi, na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) yaliyoandaliwa na shirika la Shalom Development Organization(SHADO) kwa ufadhili wa Mtandao wa Maendeleo ya awali ya mtoto Tanzania(TECDEN).
SHADO iliandaa mafunzo hayo ili kuwezesha wanahabari kuwa na uelewa wa pamoja na wao waweze kushiriki kwenye utekelezaji wa PJT-MMMAM. Kupitia kalamu zao waweze kuihimiza jamii kuiishi programu hiyo inayolenga kuwezesha ukuaji timilifu wa watoto ili kuwa na taifa lililo na rasilimali watu sahihi kwa miaka ijayo.
Mwandishi huyo anakiri wanahabari wanayo nafasi kubwa ya kuleta mapinduzi kwenye nyanja ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iwapo wataweka mkazo na kuzipa kipaumbele habari zake. Kujifunza kutoka kwa wenzao pamoja na wataalamu waliobobea kwenye Malezi ya watoto kutawapa uwanja mpana zaidi wa kuibuka na habari zinazoweza kupendwa zaidi na walaji wa kazi zao.
Anasema miongoni mwa habari zilizowahi kumvutia na kumshawishi kujikita kwenye uandishi wa habari za watoto ni pamoja na ya Ofisi ya Mwenyekiti wa Kijiji Nkung’ungu kugeuzwa Zahanati. Habari iliyoandikwa na kuchapishwa Juni 23, 2019 katika gazeti la Habarileo ikielezea mazingira yasiyo rafiki ya upatikanaji wa huduma za wanawake waliokwenda kujifungua kituoni hapo pamoja na watoto wachanga kupata chanjo.
Malo anasema utekelezaji wa PJT-MMMAM ni fulsa nyingine kwa waandishi wa habari ya kuonesha uwezo wao kwa kuyaangazia maeneo makuu matano yanayotajwa kuwa muhimu katika kusimamia ukuaji timilifu wa mtoto. Maeneo hayo ni pamoja na Lishe toshelezi, Afya Bora, Malezi yenye muitikio, Fursa za Ujifunzaji wa Awali na Ulinzi na Usalama.
Anasema yapo maeneo mengi ambayo bado yanahitaji kufuatiliwa na wanahabari ili kuiambia jamii nini kinafanyika, kinakasoro gani na kilipaswa kuwa vipi ili kiwe na tija katika ustawi wa watoto. Bado zipo mila na desturi zinazopwaswa kupigiwa kelele kwakuwa zimeendelea kuwa kikwazo kwa ukuaji wa mtoto hususani aliye katika umri wa kuanzia miaka sifuri hadi nane.
“Kujikita kwenye uandishi wa habari za watoto hakukupi sifa pekee ya kuwa mwanahabari mwenye kustahili tuzo bali pia kuwa kinara kwenye kuokoa jamii inayokuzunguka kwakuwa kalamu yako itawezesha kuleta babadiliko chanya kwenye suala la malezi.” Anasema Malo.
Suala la wadau kutoa kipaumbele kwa waandishi wa habari kujengewa uwezo zaidi na uelewa wa mazingira rafiki ya ukuaji timilifu wa mtoto ili waweze kuisaidia jamii linatajwa kuwa muhimu. Hii si kwakuwa tu wataandika habari na kuandaa vipindi wakiihabarisha jamii bali pia wakiwa sehemu ya wazazi na walezi wanaweza kuwa chachu ya mabadiliko kwenye maeneo yao kwa kuwa mfano wa kuigwa.
Nebart Msokwa ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Mbeya(MBPC) iliyo chini ya Muungano wa Klabu za waandishi wa habari nchini(UTPC), anasema yapo mambo mengi hayajafanyiwa kazi na wanahabari na huenda kutokuwa na uelewa nayo wanaona si habari. Huenda pia wao wanayaishi wakiamini yako sahihi lakini wakiojengewa uelewa wanaweza kuyaepuka na kuionyesha jamii inayowazunguka kuwa hayafai.
“Yapo mambo tumeyasikia hapa sisi wenyewe ni mapya na hatuyafanyi kwenye familia zetu tukiamini hayana umuhimu. Leo hii tunaambiwa na wataalamu hapa kuwa mtoto aliyepo tumboni anapaswa kufanya mawasiliano na baba au watu waliopo kwenye familia yake.” Anasema Msokwa.
Shukuru Mgoba mwandishi wa Gazeti la Habarileo anasema “Mimi nimekuwa nikigombana na mtoto mara nyingi kila ninapoona anaonesha nia ya kwenda kucheza, wakati wote nataka azingatie marudio ya kile alichojifunza shuleni kila aliporejea nyumbani jioni. Lakini kumbe ni muhimu pia akawa na muda wa kucheza au kuchangamana na wenzake, inamuongezea uchangamfu katika kujifunza kwake.”
Mwanahabari Keneth Ngeresi aanasema mchano wa mwandishi wa habari katika uchechemuzi wa PJT-MMMAM unahitajika kwa kiasi kikubwa. Ni muhimu kwakuwa kwa nafasi yao waandishi wa habari wanaaminiwa na jamii. Mara nyingi jambo linapotangazwa au kuchapishwa ndipo huaminiwa na watu wengi.
“Hata kukiwa na ubishani juu ya tukio lolote utasikia mmoja anasema hata redioni wametangaza, au kwenye luninga. Yote hiyo anathibitisha uwepo wa nguvu ya vyombo vya habari. Sasa sisi tukiwa na uelewa wa kutosha juu ya programu hii nina imani kuwa jamii nayo itapata habari sahihi juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(MMMAM). Hapo malengo ya serikali na wadau yatafikiwa.”
“Hapa tumesikia kuwa vile tulivyo ni kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati wa ukuaji wetu katika kipindi cha miaka sifuri had inane. Naanza kupata picha kuwa yawezekana kuna hata viongozi na wataalamu kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za serikali tumekuwa tukiwalaumu kwa kuvurunda mambo kumbe makosa yalifanyika huko nyuma.” Aliongeza Ngelesi.
Mratibu wa Mradi wa Mtoto Kwanza kutoka Shirika la SHADO lililo na jukumu la kufanya uchechemuzi wa PJT-MMMAM mkoani Mbeya, Jenipher Antony anasema wanahabari ni muhimili muhimu katika mwenendo wa malezi na makuzi ya mtoto. Anasema wadau wanatamani kalamu za wanababari zifanye kazi kwa haraka zaidi kwenye kusisitiza ustawi wa mtoto.
“Hata katika mazingira ya ukatili dhidi ya mtoto tungependa kuona wanahabari wanaihimiza jamii kutoa taarifa pale tu wanapoona mazingira yasiyo rafiki kwa mtoto. Tusisubiri kuandika habari wakati mtoto amekwishabakwa au kulawitiwa. Kama tuligundua mapema mazingira yasiyo rafiki kwake hiyo ndiyo iwe habari ya kipaumbele” anasema Jenipher.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya, Elukaga Mwalukasa anasema kwa wanahabari kujengewa uelewa juu ya PJT-MMMA anaamini utekelezaji wa programu hiyo utakuwa endelevu na hautoachwa kwa watendaji wa serikali pekee au wadau wachache. Jamii itapata msukumo kwa kupata habari mara kwa mara zinazoandikwa kwa weledi juu ya mazingira yaliyo sahihi kwa ukuaji timilifu wa watoto.