Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuibeba na kuipa umuhimu wa pekee agenda ya usafi ili kuepuka maradhi yanayosababishwa na uchafu.
Ametoa kauli hiyo leo alipozungumza na wafanyabiashara wa soko la Sabasaba katika Kata ya Ilemela,baada ya kuzuru katika soko hilo kuhamasisha jamii kujenga mazoea na tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao kwa vitendo.
“Usafi ni afya na afya ni usafi,rai yangu kwa wananchi wa Ilemela tujenge tabia ya kufanya usafi na kusafisha mazingira yetu ili kuepuka maradhi yanayosababishwa na uchafu,agenda hii ya usafi ipewe kipaumbele kutokana na umuhimu wake kiafya,”amesema Wayayu.
Mkurugenzi huyo wa Ilemela,amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa halmashauri ina mpango wa kuboresha masoko yote ya ndani ya manispaa hiyo ikizingatiwa masoko hayo ni miongoni mwa vyanzo vya mapato yanayosaidia kutoa huduma mbalimbali za kijamii.
Pia,kuhusu uwezeshaji kiuchumi kwa makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu, Wayayu amesema wafanyabiashara walionufaika kwa fedha za mkopo unaotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri,warejeshe mikopo hiyo ili fursa ya kukopa iendelee kwa wahitaji wengine na kuifanya endelevu.
Naye Diwani wa Ilemela (CCM),Wilbard Kilenzi,amesema uwezeshaji kiuchumi kwa wananchi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa makundi ya wanawake,vijana na walemavu,wawe watulivu kwa sababu halmashauri imeweka miongozo na utaratibu mzuri wa kuanza kutolewa kwa mikopo hiyo.
Awali wafanyabiashara hao wamepata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu uboreshaji wa soko hilo wakimuomba Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela kuona namna bora ya kuimarisha miundombinu ya vyoo na kulipanua soko hilo watu wengi wapate nafasi ya kufanya biashara ndani ya soko.
“Soko hili ni salama na watu wengi wanatamani kufanya biashara hapa,changamoto ni ufinyu wa eneo na uwezeshwaji wa mitaji,” amesema Mwenyekiti wa Soko la Sabasaba,Khasim Msangi.