Na Sophia Kingimali.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Mussa amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wake anaoufanya kwa kuzingatia jinsia kwani umepelekea nchi kuwa na wanawake asilimia 24 katika Diplomasia.
Pongezi hizo amezitoa wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 24,2024 jijini Dar es salaam katika maazimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake katika diplomasia ambapo kwa mara ya kwanza yanaazimishwa nchini tangu kuaasisiwa kwake mwaka 2022 na Baraza la Umoja wa Mataifa.
Amesema Rais amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanawake wamekuwa mbele katika ngazi ya maamuzi kwa kuhakikisha anawachangua katika nafasi mbalimbali za maamuzi.
“Katika kutambua mchango wa wanawake katika diplomasia leo hapa tupo na wanadiplomasia nguli kutoka ndani ya nchi na nje tunae Balozi Getrude Mongera,Balozi Amina Salum Alli,balozi Riberata Mulamula na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa”,Amesema Balozi Mussa.
Kwa upande wake Waziri wa maendeleo ya Jamii kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Riziki Pembe Juma amesema uwepo wa maadhimisho hayo hapa nchini ni jitihada ya serikali zote za Muungano katika kuhakikisha inamuwezesha mwanamke kuingia katika nyanja zote za maamuzi.
“Serikali zote mbili zimetambua uwepo wa wanawake kwa kuwachagua katika sekta mbalimbali ikiwemo mawaziri ambapo sasa kwa Zanzibar wanawake waliopo katika nafasi za maamuzi ni asilimia 33”,Amesema Pembe.
Akizungumzia kuhusu uchumi Pembe amesema serikali zote zimeweka miundombinu ya kuwainua wanawake ikiwemo kuwapa kipaumbele katika kuwapa mikopo isiyokuwa na riba.
“Wanawake wamepewa kipaumbele kila sehemu kwenye siasa tunae Jemedari wetu Rais Dkt Samia,ukienda kwenye uchumi wanawake wapo,kwenye elimu,Afya kote serikali imeweka mazingira mazuri kuhakikisha mwanamke anapata nafasi”,Ameongeza.