Jamii imeshauriwa kuwa na utaratibu malumu wa kufanya mazoezi mara kwa mara kwa lengo kuweka mwili sawa ili kujikinga na maradhi yasioambukiza.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Azzan Sports Foundation, Iddi Azzan wakati wa tamasha la michezo liliofanyika katika uwanja wa barafu uliopo Magomeni Makuti, Jijini Dar es Salaam.
‘’Bonanza hili malumu la kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi, tumeandaa sisi barafu jogging kwa kushirikiana na chama cha jogging Kinondoni (KIJA) pamoja na Wizara ya Afya’’ alisema Azzan.
Aidha, Mbunge huyo wa zamani wa Kinondoni, ameishauri jamii kufanya mazoezi kwajili ya kujikinga na maradhi yasiyo ambukiza kwakuwa mazoezi ni muhimu.
Pia, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuhamasisha jamii katika kufanya mazoezi.
‘’Mazoezi ni muhimu sana na tunapata sapoti kubwa sana kutoka serikalini kupitia Wizara ya Afya na wao wamekuwa wakitusaidia sana katika hili. Kauli mbiu yetu ya ‘Mtu Ni Afya’, lazima tuendelee nayo kwa kuwa bila afya huwezi kufanya chochote’’ alisema.
Azzan, alisema mazoezi yatasaidia kuimarisha afya kuanzia watoto mpaka watu wazima.
Naye Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe ameshukuru sana mwitiko wa wananchi kuweza kufika katika tamasha hilo.
Alisema lengo kubwa la Wizara ya Afya ni kuhamasisha ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya ‘Mtu Ni Afya’ ilizinduliwa na makamu wa Rais Wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango na kusimamiwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Alisema bado tunaendelea kufanya uhamasishaji mazoezi pekee yake hayatoshi lazima yaendane na ulaji chakula ulio sahihi.
‘’Tumekuwa tukifanya uhamasishaji wa kampeni ya ‘Mtu Ni Afya’ na kampeni imejikita katika maeneo makuu matatu ambapo moja ni kupambana na magonjwa yasiokuwa ya kuambikiza kama magonjwa ya Kisukari, Shinikizo la damu pamoja na Kansa’’ alisema.