Na Mwandishi wetu, Nzega
MKUU wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Lumeya Tukai, amekutana na watendaji wa vitongoji, mitaa, vijiji, kata na maofisa tarafa kwa ajili ya dhifa ya pamoja ya chakula cha mchana na vinywaji kwa lengo la kupongezana kwa namna wanavyoitumikia jamii.
Dhifa hiyo iliyoandaliwa na DC mhe Tukai, imewahusisha watendaji wote wa wilaya ya Nzega, yenye Halmashauri mbili za Wilaya na majimbo matatu ya uchaguzi wa ubunge.
Katika dhifa hiyo iliyowahusisha watumishi 250, wakiwemo watendaji 179 wa vijiji, mitaa 14 na kata 46, wakiongozwa na wajumbe wa kamati ya usalama ya wilaya (KU) kupitia Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), Winfrida Emmanuel Funto.
Viongozi wengine waliohudhuria dhifa hiyo ni maofisa Tarafa za Nyasa, Puge, Mwakalundi na Bukeni, meneja wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) mkoa wa Tabora, meneja wa benki ya NMB Tawi la Nzega na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
DC Nzega Mhe Tukai, akizungumza kwenye dhifa hiyo amewapongeza watumishi wote waliohudhuria kwa namna wanavyofanya kazi zao kwenye maeneo tofauti.
“Lengo ni kuhakikisha tunakuwa pamoja katika kuendeleza gurudumu la kuktoa huduma kwa wananchi wanaotuzunguka kwenye maeneo yetu ambao ndiyo mabosi wetu,” amesema Mhe Tukai.
Amewataka watumishi hao waendelee kufanya kazi zao ili mradi wasimuonee mtu yeyote naye yupo nao sambamba katika kuwatumikia wananchi wote wa Nzega bila ubaguzi.
Afisa Tarafa ya Nyasa, Ricardo Katambi Komanya, amemshukuru na kumpongeza Mhe DC Tukai kwa namna alivyoandaa dhifa hiyo ya chakula kwenye mchana huo.
“Ninampongeza Mhe DC Tukai kwa ubunifu huu kwani ni tendo la kiungwana na la upendo lenye kuwaleta pampja wafanyakazi na Serikali na viongozi,” amesema Komanya.