Naibu Mshauri wa Wanafunzi, Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Bi. Zitta Victoria Mnyanyi (kushoto) akizungumza na wachezaji wa mpira wa miguu na Pete kabla ya kuanza kwa Mashindano ya Madarasa 2024 yanayofanyika katika Viwanja vya Michezo Kituo Cha Tegeta.
Kaimu Mwalimu wa Michezo Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Bw. Joseph Ally Sule akizungumza na wachezaji wa mpira wa miguu na Pete kabla ya kuanza kwa Mashindano ya Madarasa 2024 yanayofanyika katika Viwanja vya Michezo Kituo Cha Tegeta.
Picha za matukio mbalimbali
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Kimezindua Mashindano ya Madarasa 2024 yanayoshirikisha wanafunzi kutoka madarasa tofauti chuoni hapo kwa kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu wanaume pamoja na mpira wa pete kwa wanawake.
Akifungua rasmi Mashindano hayo Juni 20, 2024 Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa Ndaki ya Dar es Salaam Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Cyriacus Binamungu, Naibu Mshauri wa Wanafunzi, Bi. Zitta Victoria Mnyanyi, amesema kuwa lengo ni kuhamasisha michezo kwa ajili ya kujenga afya ya mwili na akili kwa wanafunzi.
Bi.Mnyanyi amesema kuwa kushiriki michezo ni muhimu kwa ajili ya kujenga afya pamoja na kuimarisha uhusiano wa wanafunzi kutoka kitivo kimoja hadi kingine na kuleta tija katika kufikia malengo.
“Mwitikio ni mzuri, tumeona wanafunzi wengi wamekuwa na hamasa kubwa kwa sababu wanapenda michezo na kujiona sehemu ya Chuo, ukizingatia viongozi wa nchi yetu wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi kupitia michezo mbalimbali” amesema Mnyanyi.
Amefafanua kuwa menejimenti ya chuo Kikuu Mzumbe wanapenda michezo na kuamua kudhamini mashindano haya pamoja na kuendelea kuboresha viwanja vya michezo.
Katika ufunguzi Mashindano ya Madarasa 2024 timu ya mpira wa miguu BPA 2 na BP 3 na mpira wa Pete BAF 1 na BPA 1 zimefanikiwa kufungua pazia ya mashindano ambayo yanaendelea kutimua vumbi katika Viwanja vya Michezo Ndaki ya Dar es Salaam Kituo Cha Tegeta.