Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Dodoma.
Nayakumbuka vyema maneno ya mwalimu wangu wa somo la Uraia (Civics) miaka 20 iliyopita nilipokuwa kidato cha kwanza. Nakumbuka wakati akitufundisha mada (topic) ya Haki za Binadamu (Human Rights) alitutolea mifano ya haki mbalimbali za binadamu kama vile haki ya kusikilizwa, haki ya kuchagua na kuchaguliwa, haki ya kujiunga na taasisi uitakayo, haki ya kujieleza, haki ya kupata elimu, haki ya kucheza, haki ya kuishi, haki ya kulindwa kutaja kwa uchache.
Lakini katika mkazo wake mwalimu alituambia pamoja na kwamba haki zote za binadamu ni muhimu sana lakini haki ya kuishi (Right to life) imebeba haki nyingine zote. Kivipi? Kimsingi, binadamu anapokuwa hai anakuwa na nguvu ya kudai haki zake ili aweze kuzipata na kuzifurahia. Akatusisitiza kuwa kama ni suala la kuzipanga haki za binadamu kimtiririko kutokana na uzito wake, basi haki ya kuishi ni namba moja, nyingine zinafuata. Habari ndiyo hiyo.
Nimeyakumbuka maneno haya ya mwalimu wangu kwa kuzingatia umuhimu mkubwa wa sekta ya afya kwani sekta ya afya ni miongoni mwa sekta ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja katika kuhakikisha binadamu anapata haki ya kuishi kupitia huduma bora za afya zinazoweza kuokoa maisha yake. Huduma bora za afya zinachangia binadamu kupata haki ya kuishi na kufurahia maisha yake kwa kupata tiba na matibabu bora.
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitaja maadui watatu wa maendeleo ambao ni ujinga, umaskini na maradhi na akaweka mkazo mkubwa kwa Watanzania kupambana kutokomeza maadui hawa kwani bila kufanya hivyo, itakuwa ngumu kufikia maendeleo. Adui maradhi atatokomezwa kupitia elimu na huduma bora za afya kwa wananchi.
Kutokana na umuhimu wa kuwa na afya bora, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi zinashirikiana katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika ngazi zote yaani zahanati, kituo cha afya, hospitali za wilaya, mkoa, rufaa hadi taifa.
Huduma ya mama na mtoto ni muhimu sana kwani bila kuweka mazingira bora ya afya, kundi hili litakosa kufurahia haki ya kuishi kwani ukosefu wa huduma au huduma mbovu dhidi yao utasababisha vifo vyao, jambo ambalo serikali haipo tayari kuliona likitokea na ndiyo maana inapambana asubuhi, mchana, jioni na usiku kutokomeza vifo vya mama na mtoto kwa kuwekeza fedha nyingi ili kuhakikisha wanapata huduma bora za afya. Juhudi za kuboresha huduma ya mama na mtoto zinafanyika nchi nzima ili kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa salama kwa kupata huduma bora za afya.
Mbunge wa Chalinze (CCM) na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete kwa upande wake ameipa kipaumbele sekta ya afya, pamoja na mambo mengine, anafanya jitihada kubwa kuhakikisha ubora wa huduma ya mama na mtoto jimboni kwake inakuwepo kwa ubora na viwango vya juu.
Kutokana na umuhimu wa raslimali fedha katika uboreshaji wa huduma hiyo, Ridhiwani Kikwete kwa kushirikiana na viongozi na wadau wa maendeleo wameandaa mbio za hisani zilizopewa jina la “Msoga Half Marathon 2024” zitakazofanyika Jumamosi Juni 29, 2024, kuanzia saa 12 Asubuhi katika viwanja vya Msoga, Chalinze ili kuchangisha fedha kiasi cha shilingi milioni 700 kwa lengo la kuboresha huduma ya mama na mtoto kwenye Hospitali ya wilaya ya Msoga kwa kununua vifaa tiba vitakavyotumika kwenye wodi ya wazazi na mtoto njiti (watoto wanaozaliwa kabla ya wakati).
Mbio hizo zitahusisha umbali wa kilometa 5, 10 na 21. Kwa yeyote aliye tayari kushiriki mbio hizo anaweza kujisajili kwa kulipia gharama za usajili kiasi cha shilingi 35,000 kwa mtandao wa Tigo kupitia huduma Lipa Namba: 15840234, jina ni Msoga Half Marathon au kutuma mchango kwa benki ya CRDB, Namba ya Akaunti CRDB ni 0150882399800 jina ni Msoga Half Marathon. Kwa mawasiliano zaidi, unaweza kupiga simu kwa namba 0762 210 253 au 0782 573 880.
Lakini kwa ambaye hataweza kushiriki katika mbio hizo, yuko huru kuchangia kiasi chochote kadri alivyojaliwa na Mwenyezi Mungu kupitia simu (Lipa Namba Tigo) na benki CRDB kama zinavyoonekana hapo juu.
Upatikanaji wa fedha hizo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya mama na mtoto na hatimaye kuwahakikisha usalama na haki yao ya kuishi kupitia huduma bora za afya. Mlango uko wazi kwa mtu binafsi, taasisi, vikundi na mashirika mbalimbali kuchangia fedha ili kuboresha huduma ya mama na mtoto katika Hospitali ya Msoga jimboni Chalinze mkoani Pwani. Kwa hakika, Msoga Half Marathon ni mkombozi wa huduma ya mama na mtoto hasa katika kuokoa maisha yao.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Maoni: 0620 800 462.