Waandishi wa habari wakiwa katika mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wa kuandika habari za michezo na jinsia yaliyoandaliwa na Tamwa Zanzibar kupitia mradi wa wa maendeleo ya Michezo Afrika “SPORTS DEVELOPMENT AFRICA, EMPOWERING GIRLS THROUGH SPORTS IN ZANZIBAR” wenye lengo la kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki katika michezo unaotekelezwa kwa mashirikiano kati ya TAMWA ZNZ, Chama cha wanasheria wanawake (ZAFELA), CYD chini ya ufadhili wa shirika la michezo la Ujerumani (GIZ).
Wanafuzi kutoka skuli za Zanzibar ngazi ya Msingi wakiwa katika Mashindano ya UMITASHUMTA kwa upande wa mpira wa kikapu (netball) na mpira wa mikono(basketball) katika viwanja vya Tabora boys Mkoa wa Tabora.
…….
NA FAUZIA MUSSA,
WANAHARAKATI na watetezi wa haki za wanawake visiwani Zanzibar na Tanzania kwa jumla, wamekuwa wakiendelea na juhudi za kutaka usawa wa jinsia uzingatiwe katika mambo mbalimbali ya kijamii na kitaifa, ikiwemo ya kisiasa na uongozi.
Hata hivyo, makala hii inaangalia zaidi mitazamo ya dini juu ya ushiriki wa wanawake katika sekta ya michezo.
Wengi wanasema kuwa, licha ya dunia kuingia karne ya 21, bado ushiriki na ushirikishwaji wa wanawake na wasichana katika sekta ya hiyo ni mdogo.
Mbali ya kukosekana idadi kubwa ya wanawake katika viwanja vya michezo, hata uongozi katika sekta hiyo imetawaliwa zaidi na wanaume.
Kwa kiasi kikubwa, Bodi na vyama vinavyosimamia michezo na wachezaji, zinashkiliwa na wanaume wengi, ijapokwa mara nyengine wanawake na wasichana wanakuwa na uwezo mkubwa kuwashinda.
Bila shaka, hali hiyo inachangia kuwawarudisha nyuma wanawake kupata maendeleo kupitia michezo katika ngazi zote.
Jee Mitazamo ya kidini , kwa upande mwengine inaweza kuwa ni tatizo linalowavunja moyo wanawake wanaopenda kushiriki michezo tofauti
MICHEZO KATIKA UISLAMU
Katika Uislamu, michezo huendana na imani na haitaruhusiwa ikiwa itakuwa nje ya muktadha wa kiimani, ambapo dhana ya michezo inaainishwa na Sheria na kuundwa kwa msingi wa historia.
Wanawake wa Kiislamu hawashiriki sana michezo ikilinganishwa na wanawake wasio Waislamu katika ulimwengu wa Magharibi.
Hii yatokana na kuwa Sharia ya Kiislamu imeweka mipaka kadhaa kwa wanamichezo wa Kiislamu, ambayo hujumuisha mipaka ya sehemu za mwili yaani ‘Awrah; ambazo hazitakiwi kuachwa wazi hadharani.
Baadhi ya masharti na mipaka hiyo ni pamoja na kuwa lazima wachezaji wakiwa wanawake au wanaume, wabakie na Hijabu yaani mavazi ya kuwasitiri maungo, huku wanaume wakilazimika kuvaa nguo zinazofunika kitovu hadi chini ya magoti.
Hijabu haina maana ya vazi lilelile moja la baibui bali inajumuisha aina ya nguo za michezo ambazo zinamuweka mwanamke katika stara.
Mfano wa Aya ya Qur’an na Hadith husika ni;
“Ewe Mtume (Muhammad- SAW)! Waambie wake zako, na binti zako, na wanawake wa Kiislamu wajiteremshie uzuri nguo zao.
Kufanya hivyo kutapelekea upesi wajulikane (kuwa ni watu wa heshima) ili wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu.” (33:59).
Hata hivyo, mafundisho ya Uislamu na matini zinasema kuwa michezo ya wanawake kwa ujumla ihamasishwe ila isiende kinyume na maadili ya dini.
Mtume, (SAW), alishindana mbio na mkewe, Bi Aisha, mara kadhaa huku Aisha akiwa ameshinda mbio mara ya kwanza.
Hadith iliyonakiliwa na Tabarani kutoka kwa Jabir ambaye amemnukuu Mtume akisema, “chochote kisicho na dhikri ni laghwi isipokuwa mambo manne; (a) Kwenda baina ya shabaha mbili (wakati wa kurusha mshale), kumfunza au kumuadabisha farasi, kuchekeshana na mke, (d) kujifunza mchezo wa kuogelea. (Targhiib Wa Tarhiib juz.2 uk.389; Dar Ihya al-Turaath).
Umar ibn Al Khattwaab (Khalifa wa pili) alisema:
Uislamu unaipa michezo umuhimu wa kiafya.Michezo hiyo ni kama kuogelea na kupanda farasi ndiyo iliyosisitizwa na Hadith za Mtume, (SAW).
Kwa kuzingatia mfano huo, baadhi ya Maulamaa wa Kiislamu wametoa hoja kuwa kutoshiriki kwa wanawake katika michezo kunatokana na vikwazo vya kiutamaduni na si makatazo ya dini.
Hata hivyo, ipo baadhi ya michezo iliyoharamishwa na Uislamu ikiwemo yote inayohusisha mauaji pamoja na michezo ya hatari kama ya wababe wanaokabana na kutupana chini (Mieleka au wrestling) ambayo hata wahusika wenyewe huwatahadharisha watu wasiige kwani ni haramu kwa mujibu wa Sharia ya dini ya Kiislamu.
KAULI ZA WASOMI NA WAUMINI WA KIISLAMU
Mwanaharakati na mwalimu wa Kiislamu Ukhty Biubwa Ramadhan Said Soud, amesema Uislamu haujamzuia mwanawake kucheza michezo ya aina zote hata inayoonekana kuchezwa zaidi na wanaume.
Amesema kinachosisitizwa na Uislamu ni heshima ya mwanamke iendelee kulindwa.
Ukhty Biubwa aliongeza kusema kuwa, michezo yote ya halali wanayocheza wanaume na wanawake wanaruhusiwa kucheza, bali iwe katika hali ile ile ya uke wao bila kuathiri stara zao.
“Mwanamke wa Kiislamu anaweza kukimbia hata kuogelea ila kinachomkwamisha ni mchanganyiko kati ya wanawake na wanaume kwenye
michezo,” alieleza Ukhty Biubwa
Alisema dini hairuhusu mchanganyiko wa jinsia mbili tofauti na hata ikiwa ni wa wanawake watupu, wanapaswa kuzingatia hijabu zao.
“Haruhusiki mwanamke kumuonesha mwanamke mweziwe utupu wake,” alisema akimnukuu Mtume Muhammad (S.A.W.), na kuongeza kuwa utupu ni ile sehemu yote ya Awrah ya mwanamke.
“Kweli michezo ni afya, michezo ni fursa za ajira lakini ndio tuvuke mipaka ya Uislamu? Unataka kwenda gym unakuta kuna mchanganyiko na kama wachezaji ni wanawake watupu basi kiongozi wao ni mwanamme, hii si sawa” alifafanua.
Alifafanua kuwa hijabu ni vile kujistiri katika maungo yote yaliyoelekezwa kuhifadhiwa na kubakisha eneo la uso na viganja vya mikono tu kwa mwananmke.
Aidha kwa upande wa wanaume, ni kustiri kitovu hadi magoti yake.
Ukhty huyo alisema, endapo hijabu itazingatiwa basi michezo inaruhusiwa iwe kwa afya au maendeleo.
Alisimulia kuwa mtume S.A.W alimuoa bibi aisha(R.A) akiwa mtoto mdogo na kuwa bado anahitaji kucheza, wakati wanaenda ziara zao wakiwa wamefuatana na maswahaba wakifika sehemu mtume S.A.W huwatanguliza maswahaba zake hadi masafa ya mbali kiasi kuwa hawaonani na hapo ndipo mtume (S.a.W) huanza kukimbizana na mke wake bibi Aisha (R.A) ikiwa ni sehemu ya michezo .hiyo ni kuashiria kuwa michezo inaruhusiwa lakini kwa namna ya kumsitiri mwanamke.
Ukhty Biubwa alieleza kuwa sasa ni wakati wa Serikali kuweka mazingira rafiki ya wanawake wa Kiislamu wa Zanzibar kuweza kucheza bila kuathiri dini, heshima, utu na stara zao ili kujipatia maendeleo kupitia michezo.
“Sio kwa maendeleo tu lakini zaidi kwa afya, tunaona wanawake wanakabiliwa na msongo wa mawazo kutokana na mambo mbalimbali kupitia michezo,tunaweza kuwasaidia katika hili lakini miundombinu ya michezo ya Zanzibar sio rafiki kwa mwanamke wa Kiislamu kushiriki,” alifafanua.
“Kwa mfano juzi sisi akina mama tulikutana sehemu yenye stara tukacheza michezo yetu kama nage na kuruka kamba kutumia haki yetu ya kucheza kwa ajili ya afya. Alhamdulillah tulifurahi na kurudi majumbani tukiwa watu wengine kabisa,” alieleza.
Kwa upande mwengine, hata wanaume wanavyovaaa wanavuka mipaka ya Uislamu kwani sehemu zao za staha zinakuwa wazi ingawa wapo wanaojitambua ambao ndani ya bukta huvaa suruali ndefu za michezo zinazobana kuwapa wepesi wa kucheza.
Amina Salum Khalfan ni kiongozi wa dini katika Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam, mwalimu na afisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Anasema Uislamu umeruhusu michezo bila kujali jinsia, kwani hata Mtume Muhammad (S.A.W) alisema; “Chezeni nao watoto wenu wakiwa na umri mdogo. “Wafunzeni kuogelea, (shubaha) kurusha mishale (rimaa)na kupanda farasi.”
Ameeleza kuwa, Uislamu umehimiza michezo kutokana na umuhimu wake ila isiwe ni yenye madhara na kumtoa mchezaji katika Uislamu wake.
“Tumeelekezwa katika Uislamu kuwa, mtu asijidhuru wala kumdhuru mwengine,” alitoa mfano.
Ukhty Amina alisistiza kuwa michezo inayoruhusiwa katika Uislamu ni ile yenye maadili ambayo itaitengeneza jamii kimwili na kiakili, isiyokuwa na utovu wa nidhamu kwa mitazamo ya dini hiyo.
“Ni lazima tuchunge mipaka ya Uislamu katika kucheza na si wanawake tu hata hao wanaume wanapaswa kujistiri wakati wanapocheza,” alieleza.
“Kama wanawake tunataka haki ya kushiriki michezo, ni lazima tujipange kuhakikisha tunacheza kwa kuchunga mipaka ya Uislamu.”
Alisema wakati akiwa masomoni nchini Sudan, alishuhudia wanawake wakishiriki michezo mbalimbali kama vile kuogelea, lakini wanatengewa maeneo maalum kwa ajili yao na hawachanganyiki na wanaume.
Alisema si kwamba michezo haikubaliki katika Uislamu, bali namna inavyochezwa ndio inakwamisha wanawake kushiriki.
Mwanamama huyo alisema haiwezekani kumchezesha mtoto wa Kiislamu hasa wa kike akiwa nusu uchi, akivaa bukta inayoanika maumbile yake yakitikisika, huku akisisitiza kuwa mfumo huo haukubaliki.
Naye Kadhi wa Wilaya ya Kati, (Mwera na Chwaka) Sheikh Abdulrahman Omar Bakar amesema ushiriki wa wanawake katika michezo ndani ya Uislamu unakubalika.
Hata hivyo, alisema kuruhusiwa huko lazima kufuatane na sharti la kuchunga stara ya mchezaji husika.
“Huwezi kumvalisha mwanamke nguo fupi zenye kubana huku wanaume wakimuangalia na kumshangiria uwanjani, na kamera za televisheni zikimrikodi ili wengine walioko mbali wamuone.
“Hii ni aina moja ya udhalilishaji kwa mwanamke. Anaweza kucheza mchezo wowote hata wa kuogelea, lakini katika mazingira ya stara bila kamera za video ili kulinda na kujali utu na uke wake.
Amesema wanawake kushiriki michezo ni suala mtambuka na kila mtu anaweza kushiriki bila kujali tafauti ya jinsia, ila ni vyema kuhakikisha vitendo vya kuwadhalilisha wanawake wanapocheza vinadhibitiwa kikamilifu, vyenginevyo athari zake ni kubwa.
MTAZAMO WA UKRISTU
Mwandishi wa vitabu na mtafiti wa haki za binadamu Christopher Wilcke, anasema wanawake wanapenda michezo na dini zote zinawapa nafasi kushiriki harakati hizo.
Hata hivyo, alisema licha ya kwamba hakuna dini inayokataza wanawake kushiriki michezo bali kinachofanyika, ni wanaume wanapenda kuwakandamiza kwa kutumia nafasi hiyo kuwafungia nyumbani.
Mtafiti huyo anaongeza kuwa kupiga marufuku ushiriki wa wanawake michezoni hakutatui tatizo bali kunafanya hali kuwa mbaya zaidi.
Kwa upande wake, muumini wa Roman Katoliki Machui Wilaya ya Kati Unguja na mwanaharakati Dkt. Mathew Herman Cyprian, amesema Ukristu haujamkataza mtu yeyote kucheza ikiamini watu wote ni sawa.
Alisema hata Ukristo unahimiza michezo kwa waumini wake wote, ingawa haufanyi hivyo kwa kuhubiri wakati wa ibada.
Alifahamisha kuwa hali inaonesha ushiriki wa wanawake katika michezo kwa dini zote ni mdogo si kwa sababu ya makatazo ya dini, bali ni kutokana na mitazamo ya jamii juu michezo na jinsia.
Mathew aliwataka vijana hasa wa kike kushiriki michezo kwa malengo, na waache dhana kwamba kufanya hivyo ni kwa ajili ya kupoteza muda na mawazo.
“Michezo ni afya, ni ajira na pia ni fursa. Bali haijuzu fursa hiyo iwe kwa wanaume tu, hata wanawake wana haki ya kishiriki.” Alihitimisha.
Nae Muumini wa Kanisa Katoliki anefanyia ibada kigango cha Mtakatifu Petro na Paulo Chunga Fransisca Camilius Clement amesema mwamko wa wanawake kushiriki katika michezo bado ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa hamasa ya michezo na sio kwamba ukristu umekataza.
Alifahamisha kuwa Imani ya dini hiyo katika kanisa Katoliki haikupingana na michezo na badala yake inaunga mkono michezo yote kwa jinsia zote kwani wamekua na vikundi mbalimbali vinavyohamasisha michezo ya aina mbalimbali katika nyumba zao za ibada.
Aliongeza kuwa wanawake wengi wanacheza sana wanapokua mashuleni chini ya umri wa miaka 18 lakini kadri mwanamke anavyokuwa ndivyo anavyoachana na michezo kutokana na hali za maisha, pamoja na miji inavyojengeka.
“Katika Mitaa yetu hakuna nafasi hata ya kukimbia, na miundo mbinu ya michezo ipo mbali kwaiyo mtu kutoka eneo moja kwenda jengine kufanya mazoezi tu inakua ngumu hii pia inamkosesha mwanamke fursa ya kushiriki michezo”.aliongeza
Amesema endapo wanawake wataamua kujipanga vizuri wanaweza kushiriki mchezo wa aina yoyote kama wanavyocheza wanaume kwani hakuna mchezo ambao mwanamke hawezi kucheza
Fransisca alitoa rai kwa viongozi wa Makanisa na viongozi wa wanawake wa Imani ya kiislamu kukutana kwa pamoja kuona kwa namna gani wanaratibu michezo itakayowashirikisha wanawake kwa maendeleo huku wakizingatia stara na heshima zao kama wanawake.