Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Mohamed Lukwele akizungumza wakati wa ziara ya Mafunzo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mhe. Dormohamed Issa akizungumza na Waheshimiwa Madiwani kutoka Manispaa ya Morogoro( hawapo pichani) wakati wa ziara ya Mafunzo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Waheshimiwa Madiwani kutoka Manispaa ya Morogoro wakitembelea miradi mbalimbali inayosimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
………………..
Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe.Mohamed Lukwele leo tarehe 20 Juni, 2024 wameliza ziara ya mafunzo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na kuonesha kuvutiwa na mradi wa shule za msingi mchepuo wa Kiingereza na mfumo wa usafi wa mazingira unaohusisha wazabuni Shirika la Uchumi na Maendeleo linalomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa(SUMA JKT).
Akizungumza baada ya kumaliza ziara hiyo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe.Mohamed Lukwele amesema, wamejifunza mambo mengi lakini kubwa ni suala la usafi wa mazingira ambalo kwao ni changamoto kubwa, hata walipojaribu kulifanya kama Halmashauri na kushikisha vikundi jamii kutoka kwenye Kata zao bado limeendelea kuwa tatizo.
Mstahiki Meya huyo ameongeza kuwa tayari wameanza mazungumzo na Shirika.la Maendeleo la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) ili kukabiliana na changamoto ya usafi wa mazingira kwenye uzoaji wa taka na wanatajia ifikapo Julai Mosi mwaka mpya wa fedha wa Serikali utakapoanza wataanza kufanya kazi na SUMA. JKT.
Waheshimiwa Madiwani hao walioambatana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro pamoja na wataalam kutoka Manispaa ya Morogoro wamepokelewa na Mstahiki Meya ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mhe. Dormohamed Issa ambaye aliwaelezea jinsi ushirikiano mzuri uliopo kati ya wataalam na Waheshimiwa Madiwani unavyofanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo ya Jiji la Mbeya.
Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo Madiwani hao wamepatiwa elimu kuhusu ukusanyaji wa mapato, uanzishaji na usimamizi wa miradi mbalimbali na mfumo wa udhibiti taka ngumu na kisha kutembelea mradi wa shule ya Msingi Azimio Mchepuo wa Kiingereza na mradi wa kituo cha burudani na starehe( City Park) na siku ya pili wametembele mradi wa Dampo Nsalaga,Soko la Mwanjelwa ,Kiwanda cha Usindikaji matunda na mbogamboga.