Na. Abel Paul, Jeshi la Polisi- Arusha.
Jeshi la Polisi limesema litaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wa ndani na nje ambao wanalitegemea Jeshi hilo huku likiwataka watendaji wa Jeshi hilo kutambua maboresho makubwa yanayofanywa na Mkuu wa Jeshi Polisi nchini na kuleta matokeo Chanya kwa wananchi katika kuwapata huduma bora.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi CP Suzan Kaganda leo Juni 21, 2024 Jijini Arusha wakati akifungua mafunzo yanayoendeshwa na Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) ambayo yamehusisha wakuu wa kikosi cha usalama Barabarani Wilaya kanda ya kaskazini ambapo amewataka wakuu wa kikosi hicho hicho baada ya mafunzo kuonyesha mabadiliko katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
CP Kaganda ameongeza kuwa wakuu wa kikosi cha usalama barabarani wanapaswa kuwasimamia na kuwapa maelekezo askari walio chini yao namna bora ya kuongea na wananchi bila ya kutumia lugha ambazo sio nzuri huku akiwambia hivi karibuni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan alitoa melekezo ya kuendelea kuboresha na kutoa huduma kidigitali ili kuepusha masuala ya rushwa kwa askari wa usalama barabarani.
Aidha CP Kaganda ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wakuu hao wa kikosi cha usalama barabarani wilaya kanda ya kaskazini kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi ambapo amewataka kujipanga vyema katika kusimamia usalama wa Barabara ambazo wananchi watakuwa wakizitumia katika kushiriki zoezi la kampeni za uchaguzi utakao fanyika baadae mwaka huu.
Nae kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo atumia fursa ya mafunzo hayo kuwakaribisha katika Mkoa huo ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini nakuwaomba washiriki wa Mafunzo hayo kutembelea vivutio vilivyopo Mkoani humo.
Anselim Peter ambaye ni Mkurungenzi wa kitengo cha Uendeshaji Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi WCF amesema mfuko huo umekuwa na utaratibu wa kushirikiana na taasisi mbalimbali ambapo amebainisha kuwa awamu hii imelenga kutoa mafunzo kwa wakuu wa vikosi vya usalama barabarani vya Wilaya kanda ya Kaskazini namna ya kuchakata taarifa za ajali pindi zinapotokea na namna ya kudai fidia kwa wahanga wa ajali.