Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akieleza utendaji kazi wa taasisi hiyo katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha akiwasisitiza wafanyakazi wa taasisi hiyo kujaza taarifa zao za ya kazi za kila wiki katika mfumo wa PEPMIS wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkuu wa Hospitali ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu akichangia mada wakati wa kikao cha wafanyakazi wa JKCI kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA Agnes Kuhenga akifafanua jambo wakati wa kikao cha wafanyakazi wa JKCI kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jilala John akitoa maoni yake wakati wa kikao cha wafanyakazi wa JKCI kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Picha na: JKCI
……………….
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
20/06/2024 Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kujaza taarifa zao za kazi wanazozifanya kila siku katika mfumo wa kupima utendaji kazi wa watumishi wa umma (PEPMIS) ili kuiwezesha Serikali kufuatilia taarifa za watumishi katika mfumo huo.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge alisema Serikali imeweka mfumo wa PEPMIS ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mtumishi wa umma hivyo kama watautumia vizuri mfumo huo utawawezesha kupata manufaa mazuri ikiwemo kupanda vyeo.
“Ninawaomba viongozi katika maeneo yenu muwasimamie wafanyakazi wajaze PEPMIS kwa wakati na wale wanaopitia changamoto wafike katika ofisi ya Utawala na Rasilimali watu ili waweze kutatua changamoto wanazopitia ili wote kwa pamoja tuwe katika mstari unaotakiwa”, alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge aliwahimiza wafanyakazi hao kufanya kazi kwa pamoja, kwa weledi, kujituma na kutolalamika pia wawahudumie wagonjwa vizuri na kuwa wakarimu kwao kwa kufanya hivyo kila mfanyakazi ataona mafanikio yake kwani idadi ya wagonjwa itaongezeka na hivyo kutimiza malengo ya Taasisi hiyo.
“Kutokana na huduma nzuri inayotolewa kwa wagonjwa wetu idadi ya wagonjwa binafsi wanaotibiwa JKCI imeongezeka na kufikia asilimia 23 ya wagonjwa wote jambo ambalo linaonyesha umahiri wa taasisi katika kutoa huduma bora”.
“Idadi ya wagonjwa tunaowahudumia katika kliniki yetu maalumu ya VIP imeongezeka kutoa wagonjwa 34 na kufikia 400 hadi 500 kwa mwezi ”, alisema Dkt. Kisenge”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Ghati Chacha aliwasihi wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuwahi kazini na kufuata taratibu na kanuni za utumishi wa Umma.
Ghati aliwakumbusha wafanyakazi hao kuvaa vitambulisho vyao vya kazi muda wote wanapokuwa eneo la kazi kwa kufanya hivyo kunawasaidia wagonjwa na wasio wagonjwa kuwatambua watu wanaowahudumia.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa taasisi hiyo daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto Godwin Sharau aliushukuru uongozi wa JKCI kwa kujali maslahi ya wafanyakazi kitu ambacho kimeongeza hamasa ya ufanyaji kazi.
“Tunajivunia kufanya kazi JKCI na kuwahudumia wagonjwa wa moyo tutaendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo ili huduma hii tunayoitoa ifike katika maeneo mengi nchini”, alisema Dkt. Godwin.