Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bi. Prisca Kayombo, (watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha, walipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, wapili kushoto ni Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, wanne kushoto ni Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Mwile Kauzeni na Maafisa wengine wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha pamoja na Mratibu wa huduma ndogo za fedha mkoa wa Simiyu, Bw. Mustapha Kimomwe.
Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bi. Prisca Kayombo, nyenzo ya kufundishia elimu ya fedha, mara baada ya kufika Ofisi za Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya utambulisho ambapo timu hiyo inatarajia kutoa elimu ya fedha katika wilaya mbalimbali za Mkoa huo ikiwemo, Mji wa Bariadi, Busega, Itilima na Meatu.
Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Bi. Prisca Kayombo, fulana yenye ujumbe unaosomeka Elimu ya Fedha Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi, kwa lengo la kuendelea kuhamasisha wananchi wa Mkoa huo kuhusu umuhimu wa elimu ya fedha katika kukuza uchumi.
Baadhi ya wajasiriamali na wananchi wa Mji wa Bariadi mkoani Simiyu wakipata elimu ya fedha kwa njia ya filamu yenye maudhui mbalimbali ikiwemo madhara ya kukopa bila malengo, Umuhimu wa bima, umuhimu wa kupanga bajeti na kuitekeleza, madhara ya kukopa sehemu ambazo hazijasajiliwa, kuweka fedha kwenye vikundi vilivyosajiliwa, matumizi sahihi ya fedha binafsi, masuala ya uwekezaji na mambo ya kuzingatia kabla ya kukopa fedha, mafunzo hayo yameandaliwa na kutolewa na Wizara ya Fedha.
Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa elimu ya fedha kwa baadhi ya wsananchi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, ambapo mafunzo hayo kwa Mkoa wa Simiyu yameanza kutolewa katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi na watoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
Picha za matukio mbali mbali ya mafunzo ya elimu ya fedha katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, elimu hiyo ya fedha ilianza kutolewa maeneo ya mijini kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi wote kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa masuala ya fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedha.
…………………..
Na Asia Singano, WF, Simiyu.
Baadhi ya wananchi wa Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha iendelee kuwapatia elimu ya fedha ikiwemo namna ya kutumia fedha, uwekaji akiba, uwekezaji, na umuhimu wa bima kutokana na wananchi wengi kuendelea kudidimia kiuchumi licha ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ujasiriamali na biashara.
Wakizungumza wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika shule ya msingi Bariadi Halmashauri ya Mji Bariadi mkoani Simiyu, baadhi ya wananchi hao walisema ukosefu wa elimu ya fedha umekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo yao ya kiuchumi huku wakiipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutekeleza Mpango wake wa Kutoa Elimu ya Fedha nchi nzima.
‘’ Sasa hii ndiyo maana ya maendeleo ya kifedha, mnapotupatia elimu hii ya kifedha, hata kama ni mama aliye mzee unapompelekea elimu basi unatuinua kiuchumi ‘’ alisema Bw. John.
‘’Tunaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha ambayo imeweza kuja kutuwezesha elimu ya fedha, kuna watu wanakopa pesa na kushindwa kuelekeza kwenye kile alichokipanga, ikiwemo kununua nguo, na wengine kunywea pombe mwisho wa siku anafilisiwa‘’Alisema Bi. Witness
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, alisema programu ya utoaji elimu ya fedha ni utekelezaji wa Mpango wa Wizara wa kutoa elimu hiyo nchi nzima ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya fedha ili waweze kujikwamua kiuchumi.
‘’Wizara ya Fedha imeona kuna haja na umuhimu wa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi, kwa hiyo ilitengeneza Mpango Mkuu wa Maendeleo wa miaka kumi, mpango huo umeanzia mwaka 2021 hadi 2030, ndani ya mpango huo kumeongelewa mambo mengi ikiwemo programu ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi’’alisema Bi. Mnzava.
Naye Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Mwile Kauzeni, alisema kuwa ni muhimu wananchi kutoa taarifa juu ya ukiukwaji wa sheria unaofanywa na baadhi ya watoa huduma za fedha wasio waaminifu, ili kuondoa changamoto wanazopata katika kupata huduma za fedha.
‘’Kuhusu mikopo umiza, Benki Kuu inaangalia na inatoa maelekezo kwamba hiyo mikopo umiza ifanywaje, kwa hiyo kama kuna mtu yeyote ambaye ameenda kukopa halafu akapata matatizo, tunaweza kuyasikiliza hapa tulipo, kwa sababu pia Benki Kuu tuna sehemu ya dawati la malalamiko, kwa hivyo mtu yeyote mwenye malalamiko kuhusiana na Sekta ya fedha anaruhusiwa kuuliza swali lolote” Alisema Bi. Kauzeni
Alisema kuwa elimu hiyo ya fedha ilianza kutolewa maeneo ya mijini kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi wote kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa masuala ya Fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedh.
Baadhi ya mikoa iliyofikiwa ni pamoja na Manyara, Singida, Kagera, Rukwa, Kigoma, na sasa ikiwa ni zamu ya mikoa ya Simiyu, Shinyanga, na Tabora ambapo mikoa yote nchini inatarajiwa kufikiwa.