NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma maarufu Mwana FA amesema Tamasha la Kitaifa la Utamaduni litakuwa la kihistoria, litakusanya tamaduni kutoka mikoa yote Tanzania.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzindua tamasha hilo Julai mwaka huu katika viwanja vya Maji Maji Ruvuma na litafanyika kwa siku saba kuanzia Julai 20 hadi 27.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari Waziri Mwinjuma amesema tamasha hilo linatokana na maagizo ya Rais Samia aliyotoa mwaka 2021 akiwa Mwanza.
“Rais aliagiza kufanyika kwa tamasha la Utamaduni kila mwaka ili kurithisha Mali na Utamaduni wa kitanzania .
“Tanzania Ina utajiri wa makabila zaidi ya 120, tofauti yake inajenga Umoja na yanaunganishwa na Lugha ya Kiswahili.
” Kudumu kwa Utamaduni inategemea namna inavyorithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine na kwamba urithi wa Utamaduni ni kivutio kikubwa cha utalii, watalii wamevutiwa sana,”amesema Waziri.
Alisema tamasha hilo litakuwa tofauti na matamasha mengine mawili yaliyowahi kufanyika mwaka 2022 na 2023 kwani litakuwa na sura ya Kitaifa na litakuwa chini ya wizara husika.
Waziri Mwinjuma amesema jukumu la rasilimali fedha litakuwa chini ya Sekta Binafsi ambayo ni Kampuni ya DrumBeat Carnival (Tz) Limited itakayosaidia pia kuhamasisha tamasha liwe na hadhi.