Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila akizungumza jambo leo Juni 19, 2024 katika hafla fupi ya Uzinduzi wa Kampeni ya utoaji wa elimu kwa umma pamoja kuitambulisha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za kodi Tanzania (TOST) iliyofanyika katika Ukumbi wa Anatoglou, Dar es Salaam.
Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Bw. Erastus Mtui akizungumza jambo leo Juni 19, 2024 katika hafla fupi ya Uzinduzi wa Kampeni ya utoaji wa elimu kwa umma pamoja kuitambulisha Taasisi ya TOST iliyofanyika katika Ukumbi wa Anatoglou, Dar es Salaam.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Toba Nguvila akizungumza jambo leo Juni 19, 2024 katika hafla fupi ya Uzinduzi wa Kampeni ya utoaji wa elimu kwa umma pamoja kuitambulisha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za kodi Tanzania (TOST) iliyofanyika katika Ukumbi wa Anatoglou, Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Chama cha Washauri wa Kodi Tanzania (TATC) Hane Habibu akizungumza jambo leo Juni 19, 2024 katika hafla fupi ya Uzinduzi wa Kampeni ya utoaji wa elimu kwa umma pamoja kuitambulisha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za kodi Tanzania (TOST) iliyofanyika katika Ukumbi wa Anatoglou, Dar es Salaam.
Picha za matukio mbalimbali
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
……
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amezindua Kampeni ya utoaji wa elimu kwa umma pamoja kuitambulisha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za kodi Tanzania (TOST) ambayo ina majukumu mbalimbali ikiwemo kupokea malalamiko ya matumizi ya nguvu katika ukusanyaji wa kodi dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kampeni hiyo imebeba kauli mbiu isemayo : Kataa Ukwepaji Kodi, Kataa kodi za Dhuluma, ambayo itafanyika kuanzia Juni 19 – 27, 2024 katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo itaanzia katika Viwanja vya Mnazi mmoja Juni 19- 22, 2024 na baadaye kuamia kwenye viwanja vya Mlimani City kuanzia Juni 23, 2024.
Akizungumza leo Juni 19, 2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila, amesema kuwa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za kodi ina umuhimu mkubwa katika kuondoa malalamiko ya walipakodi nchini dhidi ya TRA.
RC Chalamila amesema kuwa suala la ulipaji wa kodi ni lazima kwa kila mtanzania wakiwemo wafanyabiashara kwani jambo rafiki katika kuchangia utekelezaji wa shughuli za maendeleo nchini.
“Katika Taifa la Tanzania mfanyabiashara amekuwa na utamaduni wa kufanya maamuzi ya kuamua Serikali ipate kiasi gani cha kodi, kutokana yeye amekuwa akiamua atoe risiti au asitoe risiti kwa mteja” amesema RC Chalamila.
Amesema kuwa uwepo wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za kodi imetokana na kuwepo wa malalamiko mengi kwa wafanyabiashara kuhusu utaratibu wa ulipaji kodi TRA, huku akisisitiza kuwa taasisi hiyo inakuja kuondoa malalamiko ya ulipaji wa kodi ili kuleta tija kwa Taifa.
“Naomba msipuuze malalamiko ya wafanyabiashara kwa kuzingatia vipindi tofauti vya msimu wa biashara ili kuleta matokeo chanya na kufikia malengo” amesema RC Chalamila.
Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Bw. Erastus Mtui, amesema kuwa kupitia kampeni hiyo ni fursa kwa wananchi na walipakodi kwa ujumla kuleta malalamiko yao katika upande wa usimamizi wa kodi, utaratibu pamoja na huduma za kodi kupitia TRA.
Bw. Mtui amesema kuwa jukumu lao ni kupokea malalamiko na kuyapatia majibu kuhusu utendaji, usimamizi pamoja sheria za TRA.
“Tuna Ofisi Mkoa wa Dodoma na Dar es Salaam, lakini kuna njia mbalimbali ya kufikisha malalamiko kwetu ikiwemo kufikia ofisini, barua pepe, kupiga simu ya bure kupitia namba 0800111022, hivi karibuni tunatarajiwa kuwa na mfumo unaotoa fursa kwa mtu kutuma lalamiko lake akiwa sehemu yoyote Tanzania” amesema Mtui.
Amesema kuwa wakati umefika kwa watanzania, walipakodi pamoja na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakipata shida bila kufahama ni wapi wanaweza kuwasilisha mlalamiko na taarifa dhidi ya TRA kuja Ofisi ya Msuluhishi kwa ajili ya kupata huduma.
Bw. Mtui amesisitiza kuwa huduma ya kupokea malalamiko na kuyafanyika kazi haina malipo yoyote anayotozwa mlalamikaji.
“Muda unaotumiwa kutatua malalamiko ni siku 30, mpango huu utarejesha uhusiano mzuri kati ya mlalamikaji na TRA, utaongeza ulipaji wa kodi kwa hiari kupitia suluhu za haki na usawa katika kutatua malalamiko’’ amesema Bw. Mtui.
Mwakilishi wa Chama cha Washauri wa Kodi Tanzania (TATC) Bw. Hane Habibu, amesema kuwa asilimia 80 ya kodi inayopatikana nchini kila mwaka inatokana na walipakodi kujikadilia wenyewe.
Bw. Habibu amesema kuwa lengo la msingi ni kuhakikisha serikali inapata kodi stahiki ili wafanyabiashara waweze kuendelea kufanya biashara na kuleta maendeleo.
“Naipongeza Ofisi ya Msuluhishi kufungua ofisi Mkoa wa Dar es Salaam, nawashauri waweke utaratibu kuwa na mkutano na wadau, wafanyabiashara mara nne kwa mwaka ili kuongeza uwelewa katika ulipaji wa kodi” amesema Bw. Habibu.
Taasisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi ujio wake umetokana na dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushughulikia malalamiko na taarifa za kodi zinazosimamiwa na TRA.
Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeanzisha kitengo huru cha kupokea malalamiko na taarifa za kodi ambacho kitakuwa kinaratibiwa na wizara hiyo, baadhi ya majukumu ya Taasisi Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi kupokea malalamiko ya rushwa dhidi ya watumishi wa TRA.
Kupokea malalamiko ya ukadiriaji wa kodi na uthamanishaji wa bidhaa usio wa haki wala uhalisia dhidi ya TRA pamoja na kupokea malalamiko ya ufunguaji wa biashara bila kufata sheria na taratibu dhidi ya TRA.