Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, Maafisa Habari wa Serikali pamoja na Taasisi mbalimbali kabla ya kufungua Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Juni, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Kamati Maalum kuhusu Kutathmini hali ya Utendaji na Uchumi kwenye Vyombo vya Habari Tanzania Bara kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mwandishi Mbobevu Tido Mhando wakati wa Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Juni, 2024.
…………………….
Na John Bukuku, Mlimani City
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suruhu Hassani amesema Serikali itaendelea kuweka mifumo ya kisera na kisheria katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa ufanisi.
Akizungumza leo Juni 18 jijijni Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari pamoja na kikao kazi cha Maafisa Habari wa Serikali lililofanyoka katika Ukumbi wa Mikutano Mlimani City ambalo limebeba kauli mbiu “Jenga Mustakabali endelevu kwenye sekta ya habari katika zama za kidijitali”, Rais Dkt. Samia amesema kuwa vyombo vya habari sio mshindani wa serikali bali ni mdau ni mshiriki muhimu wa shughuli za serikali.
Amesema kuwa vyombo vya habari ni muhimu kulisemea Taifa mambo mazuri, lakini kuna baadhi ya waandishi wahabari na vyombo vya habari vimekuwa vikiandika habari mbaya za kulitangaza Taifa.
Amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa kuripoti habari za taifa kwa weledi na kutangaza Maendeleo yaliyofikiwa.
“Nikienda Nchi za wenzetu napongezwa kwa kazi nzuri inayofanywa kwa kusimamia sekta ya habari, lakini kuna baadhi ya wanahabari hawaoni mazuri yanayafanywa na serikali”amesema Rais Dkt. Samia.
Ameeleza kuwa vyombo vya habari vikifanya kazi yake kwa uhuru vinagusa kila pembe ya taifa na kuhamasisha kupokea ujuzi mpya, taarifa za maendeleo ya teknolojia, kufichua maovu na kusaidia viongozi kupata mrejesho.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa uhusiano kati ya serikali na vyombo vya habari unazidi kuimarika, huku akibainisha kuwa ripoti za kimataifa zikionesha kuimarika kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Rais Dk.Samia amesikitishwa na tukio la mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Asmiwe Novath mwenye umri wa miaka miwili na miezi sita ambaye aliibiwa nyumbani kwao Mkoani Kagera na baadaye kupatikana akiwa amefarikia dunia huku baadhi ya viungo vya mwili wake vikiwa vimenyofolewa.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, amesema kuwa Tanzania haijafika katika uhuru wa habari unaoutarajiwa angalau ipo katika hatua tofauti na siku za nyuma.
Amesema kuwa hatua hiyo ni mageuzi ya usimamizi katika sekta ya utangazaji na mapitio ya sera na kanuni ambayo misingi wake ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia.
” Lengo la kongamano hili ni kutathmini sekta ya habari na kuweka mikakati tunakokwenda na kongamano hili ambalo ni la pili kufanyika kutakuwa na mada mbalimbali na kujadili kuondoka na maadhimio,”amesema Nnauye.
Baadhi ya Wadau mbalimbali wa Habari, Wanafunzi wa Tasnia ya Habari pamoja na Waandishi wa Habari wakiwa kwenye Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Juni, 2024.