Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akifungua Mafunzo ya Siku Nne ya BRELA kwa Waandishi wa habari ambao wanaripoti Mkoa wa Dar es Salaam, yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni BRELA (BRELA) Godfrey Nyaisa akizungumza wakati wa Mafunzo ya BRELA kwa Waandishi wa Habari wanaoripoti Mkoa wa Dar es Salaam, yaliyofanyika mkoani Morogoro.
………………
Na Sophia Kingimali.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk.Hashil Abdallah amewataka wafanyabiashara nchini kurasimisha biashara zao ili kuweza kuleta maendeleo na kukuza uchumi na kuongeza pato la Taifa.
Hayo yamesemwa leo Juni 18,2024 katika mafunzo ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa waandishi wa habari yaliyofanyika mkoani Morogoro amesema biashara zikirasimishwa zitasaidia kukuza maendeleo nchini .
Amesema katika kutafsiri kwa vitendo dhamira,mwelekeo na dira ya Dk.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kama Wizara ilikaa na kuona kuna tatizo moja la habari kutokufika kwa usahihi na habari sahihi kuchelewa kufika kwa wakati sahihi hivyo kupitia Brela wameandaa semina maalum kwa waandishi wa habari
Aidha amesema lengo la kutoa mafunzo hayo kwa waandish wa habari ni kuwafahamisha shughuli za msingi zinazofanywa na Brela,Sera za Biashara zilizopo kwenye nchi na jinsi ya kurasimisha biashara kutoka kutokuwa rasmi na biashara kwenda kuwa rasmi.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo na kuwafahamisha majukumu yanayofanywa ndani ya taasisi zao na yaliyofanywa na Komredi Jemedari Dk.Samia Suluhu Hassan katika falsafa nzima ya kuwekwa mazingira wezeshi na rahisi ya ufanyaji wa biashara nchini.
Ameeleza kuwa katika mafunzo hayo watachambua sheria sita ambazo zinasimamiwa na Brela ikiwemo miliki bunifu,usajili wa biashara,urasimishaji wa biashara wataalam wataweza kutoa elimu kwa waandishi wa habari,
“Imani yetu kwamba mafunzo haya yatawanufaisha waandishi na kutoa elimu kubwa kwa wabunifu jamii na nchi kwa ujumla juu ya urasimishaji,ufanyaji biashara na uwekaji wa mazingira wezeshi unaofanywa katika biashara na uwekezaji ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ”amesema
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema wataendelea kufanya kazi kwa karibu na waandishi wa habari ili kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi kutoka kwa wakala hao (BRELA).
Amesema mafunzo hayo ni moja ya utekelezaji wa maazimio yao ya kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma kuhusu utendaji kazi wao na kuhimiza umma kurasimisha biashara zao.
Aidha Nyaisa amesema kuwa mafunzo yatakuwa endelevu kwa waandishi wote nchi nzima ili kuhakikisha wanapata uelewa kuhusu Wakala huo lakini pia kuhakikisha waandishi wanapata taarifa sahihi kutoka kwenye chanzo husika.
“Mafunzo haya yatakuwa endelevu na tutawafikia waandishi nchi nzima kwani matarajio yetu kuwa na mabarozi wa zuri watakaoweza kuandika makala na taarifa sahihi ili kumuwezesha mwananchi kuweza kuhamasika kurasimisha biashara yake lakini pia tutaandaa tuzo kwa ajiri ya waandishi watakao wamefanya vizuri katika uandishi wa habari zinazohusu shughuli zinazofanywa na BRELA”,Amesema Nyaisa.