Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Igunga, Ebenezer Ole Mainoya.
Baadhi ya viongozi wa kata wa ccm wakimsikiliza kwa makini Katibu wa CCM wa wilaya hiyo.
…………………..
NA VICTOR MAKINDA: IGUNGA TABORA
Ikiwa imesalia takribani miezi minne kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, Ebenezer Ole Mainoya, amewataka viongozi wa ngazi zote wa hicho wilayani Igunga, kuelekeza nguvu zao kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili chama hicho kiweze kupata ushindi wa kishindo.
Mainoya ameyasema hayo, mjini Igunga, wakati wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa ilani ya CCM na mipango kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, uliowaleta pamoja viongozi wa CCM wa kata zote 16 za jimbo la Igunga ambao ni Wenyeviti makatibu wa chama na jumuiya zake pamoja na wenezi.
“ Muda ni mchache mambo ni mengi, ninawaomba ndugu zangu, viongozi wenzangu, tuelekeze nguvu zetu kwenye uchaguzi wa serikali za mita, tushuke chini kwenye matawi na mashina na kwa wanachama wetu na hata wasio wanachama wetu tukawahamasishe kwanza kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa pindi wakati utakapowadia na pili kukichagua CCM kwa kuwa chama hiki kimewatendea mengi mazuri ya maendeleo watanzania.” Amesema.
Mainoya amesema kuwa CCM wilayani Igunga, imetekeleza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa asilimia kubwa kwa kuwa miradi mingi ya maendeleo imepelekwa wilayani humo, hivyo viongozi wanayo ya kuyasema kwa wananchi.
“Chama chetu ni cha uongozi, chama cha kupigania maendeleo ya watu, tunazo hoja nyingi za kujinadi na kuwaleza wananchi kwa kuwa wilaya yetu imepata miradi mingi mikubwa ya elimu, afya, umeme, maji na miundombinu.” Amesema
Ameongeza kuwa hakuna kijiji wilayani Igunga ambacho hakijafikiwa na mradi wa maendeleo huku umeme ukiwa umefika vijiji vyote wilayani humo.
Naye Mbunge wa jimbo la Igunga, Nicholaus Ngassa, akitoa taarifa za utekelezaji wa ilani jimboni humo alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne tangu aingie madarakani amefanya jitihada kubwa kupambania maendeleo ya jimbo hilo ambao mabilioni ya shilingi yamepelekwa kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ngassa aliwaahidi viongozi hao wa kata kuwa yupo nao bega kwa bega kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na ikiwa watakwama kwa lolote mahali popote wawasiliane naye haraka.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Mafunda Temanywa, amesema kuwa wilaya ya Igunga ina jumla ya vijiji 109 na vitongozi 75, hivyo amewataka viongozi hao kushirikiana kwa karibu na kamati za ushindi walizoziunda kushinda vijiji na vitongoji vyote.