Muonekano wa kituo cha mafuta kinachojengwa katika mji wa Namtumbo wilayani Namtumbo.
Mmiliki wa kituo cha mafuta kinachojengwa katika mji wa Namtumbo mkoani Ruvuma Said Kazibure kushoto,akimkabidhi taarifa ya mradi huo ,kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava, kulia kwa Mnzava ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya.
Na Mwandishi Maalum, Namtumbo
WAKAZI wa mji wa Namtumbo hasa wanaotumia vyombo vya usafiri ikiwemo pikipiki na magari,wataondokana na adha ya huduma ya nishati ya mafuta baada ya kuanza kujengwa kwa kituo cha mafuta.
Jumla ya Sh.milioni 515 zimepangwa kutatumika katika ujenzi wa mradi wa wa kituo hicho ambacho ujenzi wake hadi sasa umefikia zaidi ya asilimia 85.
Kituo hicho kinatarajia kutatua changamoto kubwa ya uhaba wa nishati ya mafuta katika wilaya ya Namtumbo,kuongeza ajira na kuinua pato la Taifa.
Akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024,mmiliki wa kituo Said Kazibure amesema,kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi na kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa Halmashauri na Serikali kwa ujumla pindi wanapotaka kwenda kuwahudumia wananchi hasa maeneo ya vijijini.
Kazibure amesema,wazo la kuanzisha kituo cha mafuta ni baada ya kuona wananchi wengi hasa wenye vyombo vya moto katika wilaya ya Namtumbo hawana uhakika wa kupata nishati hiyo muhimu.
Alisema,katika Makao makuu ya wilaya ya Namtumbo kuna kituo kimoja kinachotoa huduma,hivyo wakati mwingine wananchi wanalazimika kwenda hadi Songea mjini umbali wa kilometa 70 kununua mafuta.
“Hadi sasa mradi huu umegharimu Sh.320,000,000,hii inajumuisha gharama za umiliki wa ardhi na vibali pamoja na gharama za ujenzi,hadi sasa ujenzi kukamilika utatumia zaidi ya Sh.milioni 515”alisema Kazibure.
Amesema,mafuta yatakayouzwa katika kituo hicho ni kwa ajili ya soko la ndani na nje ya wilaya,hasa ikizingatia wilaya ya Namtumbo inapitiwa na idadi kubwa ya malori yanayobeba makaa ya mawe na nafaka kutoka wilaya na mikoa jirani kuelekea mikoa ya Lindi,Mtwara na Dar es slaam.
Pia amesema,kituo hicho kinatarajia kutoa ajira moja kwa moja 10 na ajira zisizo za moja kwa moja zinazokadiriwa kufikia 15 na kipaumbele cha ajira kitatolewa kwa wazawa wa wilaya ya Namtumbo na sio vinginevyo.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava,amewataka wamiliki wake kuhakikisha wanafunga vifaa vyote muhimu vya tahadhari ya moto.
Amesema,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameendelea kuifungua nchi yetu kwa kuruhusu uwekezaji wa miradi mbalimbali ili kukuza uchumi na kuharakisha maendeleo ya wananchi wake.