Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya akitoa maelekezo kwa Meneja Mradi kutoka Kampuni ya kikandarasi ya STECOL, Cao XiaoJun (WaKwanza kulia) alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Malagarasi-Ilunde – Uvinza (Km 51.1), mkoani Kigoma.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis Choma akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya (WaKwanza kushoto) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Malagarasi-Ilunde – Uvinza (Km 51.1), mkoani Kigoma.
Mhandisi, Thomas Sam kutoka Kampuni ya uhandisi ushauri ya NORPLAN akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya (hayupo pichani) alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Malagarasi-Ilunde – Uvinza (Km 51.1), mkoani Kigoma.
………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amemuagiza mkandarasi STECOL anayejenga barabara ya Malagarasi – Ilunde – Uvinza (Km 51.1) kwa kiwango cha lami kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara hiyo ifikapo Machi 28, 2025.
Kasekenya ametoa agizo hilo mkoani Kigoma, Juni 14, 2024 ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza mkandarasi huyo kujipanga na kukamilisha mradi huo kwa wakati kwani mpaka sasa hakuna changamoto yeyote inayokabili mradi huo ikiwemo masuala ya fedha wala vifaa kwa mkandarasi.
“Hakikisha Mkandarasi unakamilisha kuweka lami Kilometa 44 zilizobaki kati ya 51, hatutegemei baada ya kipindi hiki wanakigoma wawe wanapita kwenye vumbi, naamini utamaliza kwa wakati kwani kila kitu unacho”, amesema Kasekenya.
Aidha, amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis Choma kuhakikisha anamsimamia Mkandarasi huyo kujenga barabara hiyo kwa ubora na kujiridhisha kila hatua ya utekelezaji wake sambamba na kutolea mfano wa barabara ya Chagu- Malagarasi ambayo imejengwa kwa ubora kwani ina miaka 10 tangu kujengwa kwake na haina kiraka wala shimo lolote hadi sasa.
Kadhalika, Kasekenya ametoa rai kwa wanakigoma na watumiaji wa barabara hiyo kuhakikisha wanatunza na kulinda alama za barabarani zitakazowekwa na kutojihusisha na vitendo vya wizi wa alama hizo kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha ajali na pia kuitia hasara Serikali.
Kwa upande wake, Meneja Miradi kutoka Kampuni ya kikandarasi ya STECOL, Cao XiaoJun amemhakishia Naibu Waziri Kasekenya kufanya kazi usiku na mchana pamoja na kuongeza wafanyakazi ili kuhakikisha wanakamikisha mradi huo kama walivyoagizwa.
Amefafanua kuwa mradi kwa sasa umefika asilimia 52 ikihusisha kazi mbalimbali ikiwemo kuweka tabaka la lami kilometa Saba, kujenga makalvati madogo na makubwa, kuweka tabaka la kokoto kilometa 9 na kuweka tabaka la udongo uliochanganywa na saruji kilometa 13.
Mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Abu Dhabi na OPEC na unajengwa kwa gharama ya Takriban Shilingi Bilioni 73.