Mmoja wa mtu mwenye ualbino akipata huduma kutoka kwa wataalamu hao walioweka kambi mkoani Pwani.
Happy Lazaro,Pwani.
Timu ya wataalamu wa uchunguzi wa saratani kutoka Taasisi ya saratani Ocean Road imeweka kambi mkoani Pwani katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya uelewa wa ualbino, ambapo kitaifa yamefanyika juni 13 ,2024 mkoani humo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Meneja kitengo cha uchunguzi wa saratani na elimu kwa umma, Dkt Maguha Stephano kutoka Taasisi ya saratani kama mdau mkubwa wa mapambano dhidi ya saratani amesema kuwa ,wanatoa huduma za uelewa wa saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino na jinsi ya kujikinga.
Aidha amesema kuwa ,huduma zingine zilizotolewa ni uchunguzi wa saratani za matiti, tezi Dume, mlango wa kizazi na Ngozi kwa watu wenye Ualbino.
“Huduma hizi zilianza kutolewa juni 11 hadi Juni 13 na kupitia huduma hiyo tunatarajia kufikia idadi kubwa ya watu wenye ualbino ili waweze kupata huduma inayotakiwa .”amesema.
Aidha Dkt.Maguha ametaja kisababishi kikubwa cha saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino ni mionzi Hatarishi ya jua.
Aidha ametaja njia za kijikinga kwa watu hao wenye ualbino kuwa ni pamoja na kuepuka shughuli za vipindi kirefu juani,kuvaa nguo zinazofunika miili kikamilifu dhidi ya mionzi ya jua,kuvaa kofia yenye kingo pana wanapokuwa juani,kutokuvaa vimini juani,kupaka mafuta ya kupunguza makali ya mionzi ya jua .
Aidha ametaja njia zingine kuwa ni pamoja na kuzichunguza ngozi zao mara kwa mara kubaini mabadiliko yoyote sambamba na kufika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi wa ngozi mara kwa mara.