Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo, jijini humu kuhusu kukamatwa kwa Yahya Ismail Nawanda, ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, akituhumiwa kulawti mwanachuo ndani ya gari. Picha na Baltazar Mashaka.
…….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Yahya Ismail Nawanda (46), amekamatwa kwa tuhuma za kumwingilia kinyume cha maumbile mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT).Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limethibitisha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC),Wilbrod Mutafungwa,amesema wanamshikilia Nawanda kwa mahojiano akidaiwa kumwingilia kinyume na maumbile,mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa),Juni 2, mwaka huu majira ya usiku huko Rocky City Malls.
Amesema Nawanda alikamatwa Juni 13,mwaka huu, majira ya saa 6:00 mchana jijini Mwanza,akidaiwa kutenda kosa hilo ambapo anahojiwa na taasisi za kiuchunguzi ukiwemo wa kisayansi.
“Tunamshikilia Yahya Ismail Nawanda,aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, mkazi wa Nyaumata,wilayani Bariadi akituhumiwa kumwingilia mwanachuo wa SAUT.Anashikiliwa kwa mahojiano na upelelezi unaokwenda sambamba na uchunguzi wa kisayansi,ukikamilika jalada litapelekwa ofisi ya mashitaka kwa hatua zaidi za kisheria,”amesema Mutafungwa.
Kuhusu waraka unaosambaa mitandaoni kuwa mtendewa wa ukatili huo ameamua kuondoa shauri hilo kwa hiari yake bila shinikizo la mtu yeyote na hataki kutumika kisiasa,amesema taarifa hiyo si sehemu ya uchunguzi wala ushahidi wao.
“Jeshi la polisi tumeona hako ka taarifa, matukio ya ukatili mlalamikaji ni Jamhuri na mtendewa ni shahidi.Taarifa hiyo ni ya mitandaoni haikupokelewa polisi na si sehemu ya upelelezi wa jalada letu,hivyo mashauri hayo ya ukatili mlalamikaji ni Jamhuri mtendewa anabaki kuwa shahidi,”amesema.
Kamanda huyo wa polisi amesema yanafanyika mawasiliano ya kulileta gari linalodaiwa kutumika kufanyika ukatili huo kwa sababu ni sehemu ya vielelezo vya upelelezi na wakati ukifika vitaoneshwa kama sheria inavyoelekeza.
“Uchunguzi unaendelea na tutachunguza pia umiliki wa gari hilo, vyombo vya uchunguzi vikikamilisha vitatupa taarifa kwa maandishi,”amesema.
Mutafungwa kuhusu taarifa kuwa wakili mmoja anyedaiwa kuingilia kati kufanya negotiation (majadiliano) na mtendewa wa tukio hilo kwamba ndio chanzo na sababu ya mwanafunzi huyo kuandika waraka huo akiomba kuondoa kesi hiyo polisi,amesema katika ushughulikiaji wa matukio ya ukatili hakuna majadiliano,msingi wake ni Jamhuri pekee.
“Makosa haya ni tofauti na matusi (mtu kutukana au kutukanwa),anaweza kufanya negotiation na si makosa yanayohusu ukatili kijinsia na watoto, hivyo hilo halijawahi kufanyika katika mazingira ya jeshi la polisi na halina uhusiano na upelelezi wa kesi yetu,”amesema na kuongeza;
“Upelelezi umekaaa vizuri na umefanyika kwa weledi wa hali ya juu katika mnyororo wa haki jinai.Subirini ukamilike mtaona kitakachofanyika,lakini kwa ushahidi wa hilo (la makubaliano) hatutaki kesi yetu iharibike.”
Aidha wakati polisi ikitihibitisha kumkamata Nawanda,tayari mamlaka ya uteuzi imeshatengua uteuzi wake ingawa taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano-Ikulu,haikueleza sababu ikiwa ni siku moja tangu kusambaa kwa taarifa mitandaoni akituhumiwa kumlawiti mwanachuo huyo wa SAUT.
Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza anayesomea Shahada ya Ugavi na Manunuzi baada ya tukio alifungua jalada polisi lenye namba MZR/CID//PE/74/2024,kitendo anachodai kufanyiwa katika maegesho ya magari ya baa ya The Cask eneo la Rocky City Malls.
Kwamba kitendo hicho alifanyiwa ndani ya gari lenye namba T496 BND, aina ya Toyota Crown majira ya usiku.sss
Wakati huohuo watu 14 wanaotuhumiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kilo 4 na mirungi kilo 64, gongo lita 22 wakiwemo wawili waliokutwa na shehena ya magunia 100 ya mifuko ya plastiki iliyozuiwa na serikali,wanashikiliwa na polisi mkoani Mwanza.
Mutafungwa aliwataja watuhumiwa waliokuwa wakisafirisha mifuko ya plastiki magunia 100 ni Abdul Issa (39) Shabir Kimwaga (33),wote wafanyabiashara na wakazi wa Bwiru,wakiwa na magari mawili yenye namba T 908 EDA aina ya Toyota Alphard na T 686 AJE,Toyota Land Cruiser.