Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha mara baada ya kufungua mkutano huo.
Posta Masta mkuu ,Maharage Chande akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo uliofanyika mkoani Arusha .
……..
Happy Lazaro,Arusha
Serikali ya Tanzania imeuhakikishia Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kuhusu msimamo wake usioyumba wa kuendelea kuunga mkono na kusaidia mipango mkakati ya Umoja huo, kwa maendeleo ya Sekta ya Posta Afrika.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akifungua mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la PAPU, unaofanyika Makao Makuu ya Umoja huo jijini Arusha.
“Kwa heshima kubwa, napenda kuthibitisha msimamo usioyumba wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kusaidia mipango mbalimbali ya PAPU,” amesema Mhandisi Mahundi.
Mhandisi Mahundi ameutaka mkutano huo wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU), kutafakari njia mbalimbali zitakazowezesha mageuzi ya posta Afrika, ili kuendana na maendeleo ya kasi ya biashara mtandao (e-commerce) pamoja na mabadiliko makubwa ya teknolojia ya mawasiliano na dijitali.
Ameongeza kuwa ,katika Afrika, Posta inafanya kazi kubwa ya kutoa huduma ya kuaminika na uhakika, na huduma yenye tija kwa biashara kubwa, ndogo na za kati (MSMEs) na ni vizuri kwamba wakati dirisha la biashara mtandao likiwa limefunguka na kuja na fursa zaidi, tayari baadhi ya Posta Afrika zimeanza kujishughulisha na kutoa huduma mbalimbali katika mnyororo wa biashara mtandao.
“bado kila mtu anakumbuka matukio ya Septemba 3 mwaka uliopita, liliposhuhudiwa tukio la kihistoria la uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Ofisi za PAPU jijini Arusha, uliofanywa na Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “
Mhandisi Mahundi amesema, tukio hilo la kihistoria la nembo hiyo, ni kielelezo na uthibitisho wa uhakika wa uongozi wa dhati na wenye maono wa viongozi wa Taifa letu kuhusu mikakati na malengo ya PAPU.
Amesema, uzinduzi wa PAPU Tower, ni alama ya juhudi za pamoja za nchi wanachama wa umoja huo, kuendeleza ugunduzi, kuimarisha mawasiliano na kukuza maendeleo katika eneo lote la Afrika.
Mkutano huo wa Baraza la Utawala la PAPU, unatarajiwa kujadili maazimio na taarifa za vikao vya Kamati za Wataalam wa masuala ya posta vilivyoanza tarehe 03 hadi 7 Juni, 2024, kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Fedha na Utawala, Sera na Kanuni, Uendeshaji na Teknolojia pamoja na Mkakati (Strategy).
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ,Nicholaus Merinyo Mkapa, amesema udhibiti madhubuti wa maafa na hatari ni muhimu katika ulimwengu wa leo hivyo Sekta ya posta lazima iwe thabiti na iwe tayari kukabiliana na majanga ya asili, vitisho vya mtandao na hatari zingine.
Mkapa amesema hiyo inahusisha kuandaa mipango ya kina ya udhibiti wa maafa na hatari, kuwekeza katika miundombinu salama, na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi ili kushughulikia dharura kwa ufanisi.
Amesema Mfumo thabiti wa sera ya posta ni muhimu kwa ajili ya kuongoza sera za mahitaji ya sekta zinazokuza uvumbuzi, ushindani na maendeleo.
Naye Postamasta Mkuu, Maharage Chande amesema kuwa ,kupitia vikao hivyo ambavyo vimeanza leo kutawasilishwa ripoti ambazo kamati zimekuwa zikifanya wiki iliyopita kwenye mambo ya teknolojia na operesheni utawala na kanuni za kiposta.
Amesema kuwa,katika kamati hizo kuna maazimio yamefanyika ya kuboresha teknolojia ,kanuni na utawala wa umoja wa Posta Afrika .
“Baada ya vikao hivi tunategemea kutakuwa na kanuni bora zaidi ambazo zitasaidia biashara, kwani kanuni za kurahisisha biashara pamoja na teknolojia zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa sana .”amesema Chande.
Mwisho.