Mkaguzi kata ya Digodigo, Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi A/INSP Matokeo Mbugano amewataka Wazazi na Walezi katika Kata hiyo kuhakikisha wanatambua vipaji vya watoto wao na kuwahimiza kuzingatia masomo yao Shuleni ili wakuze vipaji vyao zaidi.
Mkaguzi huyo ametoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea maeneo ya ufundi wa magari katika Kata hiyo na kumkuta mtoto wa darasa la nne ambaye baada ya kuzungumza nae juu ya uwepo wake maeneo hayo, alimweleza kuwa anatumia muda wake wa likizo kuongeza ujuzi katika fani ya utengenezaji wa magari ambayo anaipenda.
A/INSP Mbugano alisema kuwa anatambua umuhimu wa ujuzi ambapo amemtaka mtoto huyo kuweka juhudi zaidi katika masomo yake ya sayansi ambayo yatamjenga na kumfanya kuwa fundi mzuri katika masuala ya ufundi wa magari hapo badaye.
Sambamba na hilo, amewataka wamiliki wa gereji kuwasihi vijana wadogo kujikita katika masomo zaidi badala ya kushinda katika maeneo ya gereji ambapo amebainisha kuwa vijana wengi badala ya kujifunza fani hiyo wanaweza kujiunga na makundi mabaya ambayo yatawapelekea kujihusisha na vitendo vya kihalifu.