DAR ES SALAAM
TCB Benki imetunukiwa tuzo kwa kuwa moja ya taasisi zilizofanya mageuzi makubwa ya kiutendaji na kiuendeshaji kama ilivyoonekana katika taarifa yake ya fedha ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha (Q1).
Benki hiyo ilitangaza faida ya kiasi cha TZS bilioni 10.7 ikiwa ni baada ya makato ya kodi.
Utunukiwaji wa tuzo hiyo ulifanyika katika hafla iliyohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan. Hafla hiyo ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo taasisi na mashirika ya umma yalitoa gawio na michango yao kwa Serikali kama faida ya uwekezaji wa Serikali katika mashirika na taasisi hizo.
Katika hafla hiyo, Serikali ilipokea TZS bilioni 637 kama gawio na michango kutoka katika taasisi na mashirika hayo. Kati ya hizo, TZS bilioni 279 zilitolewa na mashirika ya kibiashara huku kiasi kilichobaki cha TZS bilioni 358 kikitoka katika mashirika na taasisi nyingine za umma. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu alieleza kuwa kiasi hicho kilikusanywa kati ya Julai 2023 na Mei 2024, huku jumla ya TZS bilioni 850 ikitarajiwa kukusanywa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.Mkurugenzi Mtendaji wa TCB Benki, Bw. Adam Mihayo akithibitisha upokeaji wa tuzo hiyo alisema,
“Sisi kama TCB Benki tunaishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa nafasi hii ya ushiriki na kujionea tukio hili la kitaifa ambalo linatutia nguvu ya kuendeleza safari yetu ya mageuzi ili kuifanya taasisi yetu kuwa benki inayoongoza kwa kuelewa mahitaji ya Watanzania.
”Ukuaji mkubwa ulioonekana unatokana na dhamira yetu ya kuboresha ufanisi na kuendelea kumridhisha mteja.
Katika safari hii ya mafanikio, tunaahidi kuendelea kuwaletea ubunifu wa kifedha unaowezesha ukuaji uchumi na mafanikio ya taifa zima,” alisisitiza.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Bw. Mchechu alieleza, “Taasisi ambazo tunazidai fedha, zile ambazo zimelipa nusu, na zile ambao hazijatoa kabisa zihakikishe kwamba zinakamilisha michango yao ndani ya mwaka huu wa fedha.
Kuichangia Serikali sio jambo la hiari au kujitolea, bali ni wajibu.” Aliongeza kuwa, “jumla ya taasisi 145 zimechangia katika kipindi hiki na hivyo kuongeza idadi kutoka taasisi 109 zilizochangia mwaka jana.”