Mwenyekiti wa TOA Taifa, Albert Msovela akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mkutano huo utakaofanyika mkoani Arusha kesho.
……..
Happy Lazaro, Arusha
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, anatarajiwa kufungua mkutano mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za MitaaTanzania (TOA).
Akizungumza jijini Arusha na waandishi wa habari Mwenyekiti wa TOA Taifa, Albert Msovela, amesema mkutano huo utafanyika Juni 12 hadi 14 mwaka huu jijini Arusha.
Amesema lengo la mkutano huo ni uboreshaji na utendaji kazi wa mamlaka za serikali za mitaa.
“Mkutano huu wenye kauli mbiu ya Boresha Msingi wa utoaji huduma za serikali za mitaa, utawashirikisha makatibu Tawala wa mikoa yote 26,wakurugenzi wa halmashauri zote 184, maofisa utumishi wa sekritqrieti za mikoa yote na halmashauri zote,”amesema
Amesema pia wamealika wakurugenzi wa manispaa zote na wasimamizi wa mamlaka za serikali za mitaa kwa upande wa Zanzibar, kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na ushiriki wa utoaji huduma kwa wananchi kupitia mamlaka za serikali za mitaa.
“Maboresho haya ya serikali za mitaa unalenga ugatuaji wa madaraka kwenda kwa wananchi,ukiwemo usimamizi wa mapato na utoaji wa huduma, za kijamii ikijumuisha rasilimali watu na ukusanyaji wa mapato,”amesema.
Aidha amesema umoja huo ulianza mwaka 2002 kwa kushirikiana na Serikali ya Japani, kupitia Shirika la Maendeleo la kimataifa la Japani (JICA) ambapo watumishi zaidi ya 6000 wamenufaika kwa kupata mafunzo kupitia TOA.
Msovela amesema katika mkutano huo mada mbalimbali zitatolewa na maofisa wabobezi wastaafu na waliopo serikalini.