Wakina mama wakipanda mikoko.
Ofisa Uvuvi Wilaya ya Pangani, Joel Mabagale akifafanua jambo kwa wageni waliotembelea kitalu cha mikoko kilichopo Kumba Mtoni.
Wadau wa mazingira wakiwa ziarani Mto Pangani.
Mdau wa mazingira Sidi Mgumia.
Mikoko
………………..
NA SIDI MGUMIA, PANGANI
Sasa ni dhahiri kwamba joto linaoongezeka duniani kwa kiwango chakutisha, na kwamba athari zake zinaonekana katika miji ya mwambao wa Tanzania.
Kiuhalisia ongezeko la joto linasababisha mvua zisizo tabirika ambazo huleta ukame wa muda mrefu na kuongezeka kwa mafuriko yanayoleta madhara katika ulinzi wa chakula na matukio mengine ya hali ya hewa (kama vimbunga) ambayo yamesababisha madhara makubwa ulimwenguni.
Jinsi athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyoonekana ulimwenguni, uelewa juu ya ugumu wa janga hili na jinsi linavyoathiri mazingira, unaongezeka.
Juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali, wanajamii lakini pia watetezi wa haki za mazingira na mashirika, ambao wanaangazia kuhusu janga la hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanawake ambao wamekua mstari wa mbele katika kupinga janga la mabadiliko hayo na kulinda haki ya mazingira salama.
Bila kubaki nyuma, wanawake wa Pangani Magharibi waliopo kwenye kikundi chenye watu 25 cha Umoja wa Usimazi wa Rasilimali za Bahari (BMU) wameamua kuwa sehemu ya harakati hizo kwakua wanatambua kwamba kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye namna ambavyo uchumi na jamii inavyoendeshwa.
Katika ziara ya hivi karibuni mjini Pangani, wadau wa mazingira kutoka taasisi mbalimbali nchini kikiwemo Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa mwaliko wa Shirika la Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) walishuhudia wakina mama hao wakiendelea na harakati za kupanda miti aina ya mikoko katika fukwe ya eneo la Kumba Mtoni ikiwa ni moja ya njia ya asili yakulinda na kuhifadhi ardhi.
Akizungumzia mradi huo ambao unafanyika katika eneo linalomilikiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na kufadhiliwa na IUCN na Ubalozi wa Ireland, Melina Julius ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha alisema wanautegemea sana mto Pangani katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku, wanawake wengi wanafanya biashara ya samaki kwa hivyo wanamini kabisa kuuharibu mto kutawaathiri wao moja kwa moja na ndio maana walioona haja ya kujumuika katika mradi huo wa uhifadhi ili kuhakikisha mto unabaki salama na kuendelea kukuza vipato vyao.
“Sisi tunategemea uvuvi kupitia mto Pangani na kwenye mikoko ndiyo mahali ambapo uzalishaji wa samaki hufanyika, iwapo mikoko itaharibiwa, kuna uwezekano wa kushuka kwa uchumi wetu hivyo tumejikita kwenye uhifadhi huu kama sehemu ya mradi wa maendeleo ya Pangani ,” na wana Pangani kwa ujumla,” alisema Julius
Aliongeza kuwa Pwani ni eneo hatarishi kwa uharibifu wa mazingira, wao kama wana Magharibi wamejitolea kuipanda mikoko hiyo kwa wingi kwakua pia inasaidia kunyonya hewa ya ukaa zaidi kuliko miti ya kawaida ikiwa ni sehemu yakupambana na uharibifu wa hali ya hewa.
Naye Katibu wa BMU ya Pangani Magharibi, Fatuma Miaji alisisitiza kuwa wanajivunia kikundi chao kwakua ni kikundi endelevu na kama wanawake kipaumbele chao ni kuyatunza mazingira na kwakua wanaihifadhi miti hata viumbe wadogo wadogo wanazaliana lakini pia kupanda miti kuna manufaa kwao kama kupunguza nguvu ya maji kuja kwenye ukuta na kuleta hewa nzuri.
“Mikoko ni ya muhimu sana na ina manufaa kwa ikolojia ya mashamba na ya bahari. Husaidia kuwepo kwa bayoanuwai na kuwa makazi muhimu ya kuzalishia samaki na viumbe vingine.Mikoko pia hufanya kazi ya kukabiliana na mafuriko, mawimbi baharini na mmomonyoko wa udongo. Mchanga wake huweza kumeza hewa ya ukaa na kukabiliana na changamoto ya hali ya hewa,” alisema Miaji
Kwa upande wake, Ofisa Uvuvi Wilaya ya Pangani, Joel Mabagale alisema wanakikundi hao walipata uwezeshwaji kutoka Shirika la IUCN kiasi cha fedha milioni 16 zikijumuisha mafunzo na mambo mengine, wameweza kutengeneza vitalu vitatu vya mikoko vyenye miche zaidi ya 10,000 lakini pia wameza pia kuchonga mizinga 20 ya nyuki ambayo imewekwa kwenye mikoko.
“Kwenye suala la uhifadhi wa kurejesha mikoko wako vizuri, wamejitahidi kupanda mikoko kwenye ukuta wa mto Pangani lakini kuimarisha ulinzi kuzuia ukataji wa mikoko na kiukweli kazi zao zinatambulika,” alisema Mabagale
Kutambulika kwa juhudi hizo za kazi ambayo waliinza tangu 2017, kumeifanya Halmashauri ya Wilaya ya Pangani iwape uwakala wa kukusanya mapato ya Halmashauri, na kasha kupewa aslimia 10 ya pesa inayorudi kwa ajili yakuwasaidia katika shughuli zao.
Mabagale alisema kuwa pamoja na mambo mengine kitu ambacho kimekuwa kikiwaangusha ni ukosefu wa sheria ndogo kwasababu zinakwamisha shughuli za uhifadhi lakini wanawashukuru IUCN kwakuunga mkono hoja na sasa wako kwenye mchakato wakuunda sheria hizo ambazo zitakapoanza kutekelezeka faini zitakuwa zinaingia kwenye mfuko wa kikundi, hivyo kuongeza kipato lakini kupata nguvu ya kupambana na wahalifu.
Hawajaishia hapo, wakina mama hao wamekuwa wakitoa elimu kwa wengine mjini Pangani juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira lakini pia kuwahimiza kuipanda na kuitunza miti kwa maendeleo endelevu jambo ambalo wanasema limekuwa na matokeo chanya kwakua watu wanaelewa na kushiriki suala la uhifadhi kikamilifu na kwa bidii.
Shirika la IUCN kwa kushirikiana na mashirika mengine linalenga kushawishi, kutia moyo na kusaidia jamii ulimwenguni kuhifadhi maliasili na kuendeleza mapambano ya kimataifa ya kuokoa viumbe hai kutokana na kutoweka.