Afisa masoko wa Kampuni ya uzalishaji wa nyama na soseji ,Henry Mosha akizungumza na waandishi wa habari kuhusu bidhaa wanazozalisha.
Wateja wakijionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na kampuni hiyo .
………..
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.Wananchi wametakiwa kuwa na desturi ya kununua bidhaa zinazozalishwa na wazawa hapa nyumbani ili kuweza kuwawezesha wawekezaji wa ndani kukua na hatimaye kuweza kuuza nje ya nchi .
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Afisa masoko wa Kampuni ya uzalishaji wa nyama na soseji ya Kilimanjaro Premium Meat iliyopo wilayani Longido ,Henry Mosha wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
Amesema kuwa, kumekuwepo na baadhi ya wananchi kutopenda kuagiza vitu vya nyumbani badala yake wanaagiza nje ya nchi kwa gharama kubwa na hivyo kuikosesha serikali mapato yake kwa kununua nje ya nchi.
“Tunaomba sana wananchi wawe na desturi ya kununua vitu vya hapa nyumbani ambavyo vinatengenezwa na wazawa kwani ni vizuri na vina ubora wa hali ya juu na kwa kufanya hivyo tutaweza kuharakisha shughuli za maendeleo katika nchi yetu.”amesema Mosha .
Aidha ameongeza kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikizalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu ambapo inazalishaji bidhaa halali kwa matumizi ya watanzania.
Mosha amefafanua kuwa,wamekuwa wakichukua ng’ombe hapa hapa Tanzania kwa ajili ya kutengeneza bidhaa hizo zinazotokana na Mifugo hiyo ambapo soko kubwa lipo katika mikoa ya Arusha na ,Dar es Salaam.
“Bidhaa zetu ni nzuri na zina ladha halisi ya nyama ya ng’ombe hivyo nawaomba wateja wasisite kutumia bidhaa zetu kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwani zinatengenezwa kwa kufuata kanuni na ubora wa hali ya juu.”amesema Mosha.
Hata hivyo amesema kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikiandaa bidhaa zake kwa kufuata usafi wa hali ya juu kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizopo kwani inajali kwa kiasi kikubwa afya ya walaji kwa ujumla.