Na Sophia Kingimali.
Viongozi wa dini waiomba serikali kuufungia mtandao wa X(Twitter) nchini kwani mtandao huo umeonekana ukivunja maadili na taratibu za nchi kwa kuhamasisha ushoga na usagaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11,2024 Mwenyekiti mstaafu wa baraza kuu la kiislam BAKWATA Khaji Sule amesema kufuatia na Dunia kuingia katika utandawazi kumepelekea kumomonyoka kwa maadili na kupelekea kuharibu taswira ya nchi.
Amesema mtandao huo umekuwa ukihamasisha mapenzi ya jinsia moja na ushoga jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Mtanzania.
“Tunawajibu wa kuyapima mambo ambayo tunaletewa ambayo yapo kinyume na maadili tunapaswa kuyapinga vikali ili kulinda maadali na tamaduni zetu za Kitanzania na kulinda kizazi kilichopo sasa na kijacho”,Amesema.
Kwa upande wake Askofu Allen Siso amesema madhara yanayotokana na kuruhusu mtandao huu kwa jamii ni kukosa kizazi chenye maadili na kuvunja tamaduni za nchi.
Amesema Serikali kupitia Bunge na wizara husika kuchukua hatua za haraka kuufungia mtandao huo ili kulinda tamaduni na maadili ya nchi lakini pia kufuata maandika ya neno la Mungu ambayo yanapinga vikali vitendo hivyo vya usagaji na mapenzi ya jinsia moja.
Alfonce Mwinga ambae ni kijana anaejihusisha na mitandao ya kijamii ametoa rai kwa vijana kutumia mitandao kwa faida lakini si kwa ajili ya mambo yasiyofaa ambayo yapo kinyume na maadili lakini pia serikali kuungalia kwa makini mtandao huu kwani unaenda kuangamiza taifa.
Munira Njau Mwalimu wa shule ya msingi Gongolamboto ametoa rai kwa wazazi kuhakikisha watoto hawashiki simu na kuingia kwenye mitandao ya kijamii kwani watoto wengi wamekuwa wakiinga kila kitu wanachokiona kwenye mitandao hiyo.