Na Sophia Kingimali.
Umoja wa Vijana Chama cha Mapinduzi(UVCCM) wameiomba serikali kupitia upya maudhui yanayorushwa na mitandao ya kijamii ambayo yanaenda kinyume na maadili na utamaduni wa nchi.
Akizungumza na waandishibwa habari leo Juni 11,2024 Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Mohammed Kawaida amesema kumekuwepo na uvunjifu wa maadali unaofanywa katika mtandao wa X yaani Twitter wa kuhamasisha ushoga na mapenzi ya jinsia moja.
“Kama jumuiya tunaitaka serikali kupitia wizara husika kufungia mtandao huu kutokana na maudhui yake kwani yapo kinyume na maadili yetu kama nchi”,Amesema Kawaida.
Amesema mtandao huu ulikusudia kabisa kuwepo kwa maudhui hayo kwa kuubadilisha jina na kutoka twitter na hatimae kuuita X ili kuwaanda watumiaji kisaikolojia.
“Huu mtandao umefika wakati sasa wakuondoka hapa nchini kwetu tunaomba mamlaka husika kushughulikia hili na sio kwa X pekee hata mitandao mingine inayochochea uvunjifu wa utamaduni wetu”,Amesema na kuongeza kuwa
“Tulipata sitofahamu baada ya kuona huu mtandao wa twitter kubadilishwa jina na kuitwa X inamaana walishajipanga kufanya hili sasa wakitaka mtandao huu ubaki nchini basi wabadilishe maudhui yake la sivyo tunaiomba serikali wauondoe huu matandao”.
Kwa upande Katibu mkuu wa chama cha Alliance for Democract Change (ADC) Doyo Hassan amesema ili kuondoa mtandao huu wa X nchini wananchi wanapaswa kujiondoa kwenye mtandao huo ili kutokuona maudhui hayo.
Amesema hatua ya kwanza kuweza kuuondoa mtandao huo ni watumiaji kuacha kabisa kuufuatilia wakati serikali ikichukua hatua zaidi ya kuufungia hapa nchini.
“Nchi yetu inamaadili lakini pia tuna hofu ya Mungu hatupaswi kuyafumbia macho mambo ambayo yatatuharibia utamaduni wetu na mila sio lazima huu mtandao kuwepo hapa nchini kwetu”,Amesema Doyo.